• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Hofu ya kupoteza kazi Bandari yaweka umoja wa viongozi wa pwani kwenye mizani

Hofu ya kupoteza kazi Bandari yaweka umoja wa viongozi wa pwani kwenye mizani

NA WAANDISHI WETU

MIPANGO ya serikali ya kitaifa kuruhusu wawekezaji wa kibinafsi kusimamia sehemu za bandari za Mombasa na Lamu, imeibua upya swala kuhusu umoja wa viongozi wa kisiasa Pwani.

Haya yamejiri huku viongozi wa upinzani katika eneo hilo wakitoa changamoto kwa wenzao wanaoegemea Kenya Kwanza kupinga hatua hiyo ya serikali.

Katika utawala uliopita wa aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta, wanasiasa wa pande tofauti Pwani walionekana kuungana kupinga jaribio sawa na hilo.

Baadaye, suala hilo liliibuka kuwa kuu la kisiasa kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu ambapo wanachama wa Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, walimkashifu Bw Kenyatta na wandani wake katika Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wakidai walipanga kuuza bandari ya Mombasa.

Katika vikao vya wanahabari na vilevile kwa mikutano ya hadhara, wanasiasa wa Kenya Kwanza walidai kuwa, viongozi wenye ushawishi katika Azimio walitaka kujinufaisha kibinafsi kutoka kwa mipango ya kubinafsisha bandari, mbali na kampuni ya Dubai Port World FZE ambayo pia ilitarajiwa kupewa usimamizi wa sehemu ya bandari.

Mwaka mmoja baadaye, na kikosi hicho kikiwa ndani ya serikali, Mamlaka ya Bandari za Kenya imetangazia wawekezaji nafasi ya kusimamia sehemu muhimu za bandari za Lamu na Mombasa.

Sehemu hizo zinajumuisha gati, eneo maalumu la kiuchumi na kituo cha kontena za mizigo.

Mnamo Jumatatu, mkutano ulioitishwa na mwenyekiti wa Kundi la Wabunge wa Pwani, Bw Danson Mwashako, kujadili suala hilo, ulishindwa kupata mwelekeo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wabunge wachache wakiwemo wa Changamwe, Bw Omar Mwinyi (ODM), mwenzake wa Matuga, Bw Kassim Tandaza (ANC), wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya (UDA), na wa Mvita, Bw Masoud Machele (ODM).

“Tumekubaliana kukutana tena baada ya wiki mbili tutakapokuwa tushashauriana na wadau wote. Hatuna kitegauchumi kingine chochote kikuu hapa Pwani isipokuwa bandari. Kabla uamuzi wowote ufanywe kuhusu kubinafsisha bandari, tutafanya mikutano na wadau hadi tutambue kile ambacho Wapwani wanataka,” akasema Bw Mwashako.

Mwishoni mwa juma lililopita, Bw Mwinyi, aliwaomba viongozi wa Pwani kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuzungumza kwa sauti moja ili kulinda rasilimali za ukanda huo na kuinua maendeleo.

Bw Mwinyi alisema, wanasiasa katika maeneo mengine huweka kando tofauti zao za kisiasa wakati wowote kunapokuwa na hitaji la kutetea maslahi ya wakazi wa maeneo wanayoongoza lakini hilo huwa halionekani sana Pwani.

Alitoa mfano wa eneo la Magharibi ambapo serikali ilibadili msimamo wa awali wa kubinafsisha viwanda vya sukari baada ya pingamizi kali kutoka kwa wanasiasa.

“Katika eneo la Magharbi, viongozi walisimama imara, wakaamua kuweka kando siasa na kuzungumza kwa sauti moja na Rais aliwasikiza,” akasema mbunge huyo.

Viongozi wanaopinga mipango ya kubinafsisha bandari wamesema mpango huo haufai kwa sababu bandari imekuwa ikipata faida, tofauti na mashirika mengine ya umma yaliyolengwa kubinafsishwa.

Rais Ruto aliweka kipaumbele kwa ubinafsishaji wa mashirika kadha kama njia mojawapo ya kuhifadhi pesa za umma.

Hatua hiyo iliungwa mkono na Hazina ya Kimataifa ya Fedha (IMF), ambayo ilisema ni mpango mzuri utakaowezesha serikali kupunguza fedha zinazotumiwa kufadhili mashirika ambayo hupata hasara kila mara.

Viongozi wengine ambao waliunga mkono kauli za Bw Mwinyi ni Seneta wa Mombasa, Bw Mohamed Faki, Mbunge wa Kisauni, Bw Rashid Bedzimba na Spika wa Bunge la Kaunti, Bw Aharub Khatri.

Waliitaka serikali ieleze Wapwani kwa nini ina lazima kubinafsisha sehemu za bandari ya Mombasa ilhali ni shirika linalopata faida ya mabilioni.

Walieleza wasiwasi pia kuhusu hatima ya maelfu ya Wapwani ambao wameajiriwa na shirika hilo la serikali.

Bw Mwashako awali aliiomba serikali ipange mkutano na viongozi wa ukanda huo ili washauriane kuhusu suala hilo.
Aliongeza kuwa, viongozi wa Pwani wataungana ili kuhakikisha kuna uwazi katika masuala yanayohusu usimamizi wa rasilimali muhimu za eneo hilo.

Spika wa Bunge la Taifa, Bw Moses Wetang’ula, alihimiza viongozi wa upinzani watumie demokrasia kueleza masuala yoyote ambayo wangependa serikali iangazie.

Alipokuwa Changamwe wikendi, Bw Wetang’ula, aliongeza kuwa, serikali ya Rais Ruto imejitolea kuwasikiza na kutekeleza maoni yao.
Wanasiasa wa Pwani wanatarajiwa kukutana na wadau wa bandari wakiwemo wataalamu na maafisa wa KPA ili kutafuta mwafaka.

  • Tags

You can share this post!

Harambee Starlets waelekea nchini Cameroon kumenyana na...

El-Nino: Wakazi sasa watakiwa kuhamia maeneo salama

T L