• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Hospitali ya Kenyatta yapewa jina la Kibaki mjini Nyeri

Hospitali ya Kenyatta yapewa jina la Kibaki mjini Nyeri

NA IRENE MUGO

JENGO la Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta eneo la Othaya, Ijumaa lilibadilishwa jina na kuitwa Hospitali ya Mwai Kibaki, kabla ya mazishi ya kitaifa ya rais huyo wa tatu wa Jamhuri ya Kenya.

Hatua hiyo ya kumkumbuka rais Kibaki kwa kuipa hospitali hiyo iliyogharimu sh1 bilioni jina lake, ilifikiwa baada ya ushawishi mkali wa maafisa wa serikali.

Haya yamejiri licha ya Bw Kibaki kukataa mapendekezo ya hospitali hiyo, kupewa jina lake.

Kinara wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka alifichua kuwa mwendazake pia, alikataa mapendekezo ya barabara ya ‘Thika Superhighway’ kupewa jina lake.

“Rais barabara hii yapaswa kupewa jina lako. Ni mojawapo ya miradi mikubwa ya maendeleo uliyofanya,” Bw Musyoka alielezea Taifa Leo katika mahojiano mnamo 2019.

Kulingana na Bw Musyoka, rais Kibaki alikataa pendekezo hilo.

Alieleza kuwa barabara hiyo kuu, ilipaswa kupewa jina la kule inakoelekea.

“Rais Kibaki alinishangaza sana na unyenyekevu wake. Hakutaka kitu chochote kipewe jina lake. Nilidhani ni pendekezo zuri nlipomwambia, japo akalitupilia mbali,” alisema Bw Musyoka.

Hospitali ya Mwai Kibaki kama itakavyotambulika kutoka leo Jumamosi, ina vitanda 35 vya kuwalazia wagonjwa.

Mradi huo ulianzishwa na rais Kibaki kuwaondolea wakazi wa Nyeri mzigo wa kusafiri hadi jijini Nairobi kwa rufaa.

Hospitali hiyo itatibu magonjwa ya mtindo wa maisha kama vile shinikizo la damu, kisukari, saratani miongoni mwa magonjwa mengine yanayosumbua watu.

You can share this post!

Sababu ya mizinga 19 kufyatuliwa badala ya 21

Mwai Kibaki (1931-2022): Ni heshima za mwisho

T L