• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Hospitali ya watoto ya Gertrude’s yaahidi kuboresha huduma

Hospitali ya watoto ya Gertrude’s yaahidi kuboresha huduma

NA LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya watoto ya Gertrude’s imeahidi kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa.

Mnamo Jumamosi, Mei 20, 2023 hospitali hiyo iliongoza matembezi ya kuchangisha fedha za kusaidia watoto wanaopata maradhi ya saratani.

Matembezi hayo yaliyofanyika jijini Nairobi yalijumuisha wafanyakazi wa hospitali hiyo na familia kadha.

Fedha zilizopatikana zitatumika kugharimia matibabu ya watoto wanaougua saratani.

Dkt Robert Nyarango alisema mbali na kukusanya fedha, matembezi hayo yalitoa fursa nzuri ya kuhamasisha wananchi kuhusu maradhi ya saratani kwa watoto lakini pia kwa watu wazima.

“Ni vyema kupima watoto kwa sababu asilimia 80 ya maradhi haya yakigundulika mapema yanaweza kutibika bila shida,” akasema Dkt Nyarango.

Naye Dkt Thomas Ngwiri ambaye ni mkuu wa kitengo cha matibabu katika hospitali hiyo alisema kugundua saratani mapema ni muhimu ili kurahisisha matibabu.

“Mpango huo wa kutibu watoto wa saratani ulizinduliwa rasmi mwaka wa 2019 na umeendelea kwa miaka mitano mfululizo,” akasema Dkt Ngwiri.

Dkt Ngwiri alisema hospitali hiyo itafanya juhudi kuona ya kwamba inafanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Nairobi pamoja na serikali kuu ili kuhudumia wagonjwa kwa njia inayofaa.

“Tunapongeza familia zilizojitolea kushiriki matembezi hayo. Tunajua tutafanikiwa katika malengo yetu,” alisema Dkt Ngwiri.

Hospitali hiyo inahudumia watoto wagonjwa kutoka Kenya na nchi jirani. Hutibu wagonjwa wapatao 300,000 kila mwaka.

Hospitali kuu ya Gertrude’s eneo la Muthaiga jijini Nairobi ina vitanda 100 vya wagonjwa wanaozuru kupokea matibabu.

  • Tags

You can share this post!

Mabilioni kuungua Huduma ikitemwa

Mudavadi awasihi mahasla wavumilie ushuru wa juu

T L