• Nairobi
  • Last Updated December 6th, 2023 9:00 PM
Mabilioni kuungua Huduma ikitemwa

Mabilioni kuungua Huduma ikitemwa

NA BENSON MATHEKA

SERIKALI itatumia mabilioni kuanzisha kitambulisho cha kidijitali cha kitaifa hata kabla ya kadi ya Huduma Namba iliyoanzishwa miaka minne iliyopita kuanza kutumika wakati ambao gharama ya juu ya maisha imelemea mamilioni ya watu.

Jana Jumatano, serikali ilitangaza kuwa, Wakenya watakuwa na kitambulisho kipya cha dijitali cha kitaifa kuanzia Septemba 16, 2023.

Mnamo 2019, serikali ilisajili Wakenya kupata Huduma Namba kwa gharama ya Sh10.6 bilioni kwa lengo ya kuimarisha usalama na utoaji huduma kwa raia wote.

Kadi hizo zilianza kutolewa kwa waliojisajili mnamo 2020 kupitia machifu na kufikia sasa, kuna mamilioni ya watu ambao hawakuzipata.

Wakati wa usajili, Wakenya walichukuliwa alama za kibaiometriki ambazo serikali ya Kenya Kwanza inasema, inalenga katika kitambulisho kipya inachopanga kuzindua kuanzia Septemba 16, 2023.

Rais William Ruto jana alitangaza kuwa, serikali yake itazindua mfumo mpya wa usajili wa kidijitali utakaopatia watu wote wanaozaliwa Kenya nambari ya kipekee ya kuwatambua.

“Mfumo huo mpya ni lazima utoe nambari ya kipekee ya kutambua wakati wa kuzaliwa kwa watu wote waliozaliwa Kenya,” akasema Rais.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Profesa Kithure Kindiki na Katibu wa Idara ya Uhamiaji na Usajili wa watu, Dkt Julius Bitok wamefichua kwamba, Serikali itaimarisha kitambulisho cha kitaifa kuwa na alama zaidi za usalama za kibaiometriki katika mfumo mpya inaopanga kuanzisha.

Bw Bitok alisema serikali inatarajiwa kuanzisha vitambulisho vipya Septemba 16, 2023, hatua aliyosema inalenga kutimiza ajenda ya Rais William Ruto ya kufanya huduma 5000 za serikali kuwa za kidijitali.

“Tunazungumzia nambari spesheli ya kibinafsi (UPI), tumetambua Septemba 16 kama tarehe ambayo serikali itaweza kuanzisha baadhi ya shughuli za kufanikisha UPI ambayo itakuwa msingi wa kitambulisho cha dijitali,” akasema katibu Bikot.

Rais Ruto alisema mfumo mpya unalenga kurahisisha huduma, kupiga vita ufisadi na kuhakikisha raia wanatambuliwa kulingana na maeneo wanayoishi.

“Mfumo mpya utaweza kupatia watu wote wanaozaliwa Kenya nambari ya pekee ya kibinafsi, kuimarisha mfumo wa sasa wa usimamizi wa kitambulisho cha kitaifa kuwa mfumo wa kidijitali wa kitambulisho cha kitaifa,” kiongozi wa nchi alisema akifungua kongamano la ID4Afrika.

Licha ya kufanana na Huduma Namba, Waziri wa Tekinolojia, Habari na Uchumi Dijitali Eliud Owalo anapuuza uwezekano wa Serikali kufufua au kuimarisha kadi hiyo iliyoanzishwa na utawala wa Jubilee. Jumula ya Wakenya 37.7 milioni walisajiliwa kupata Huduma Namba.

Serikali pia imeanzisha leseni za dijitali za kuendesha magari, mradi uliogharimu Sh2.1 bilioni.

Jana Jumatano, Bw Kindiki alisema serikali itaanzisha mfumo wa dijitali wa kitambulisho kipya kama njia moja ya kutambua watu wote wanaozaliwa Kenya na kurahisisha huduma.

Akizungumza katika kongamano la ID4Afrika lililofunguliwa na Rais William Ruto jijini Nairobi jana, Profesa Kindiki alisema kitambulisho hicho kipya kitakuwa na alama zaidi za usalama ili kukabiliana na masuala yanayoibuka. Kwa wakati huu, alama ya usalama katika kitambulisho cha kitaifa ni ya kidole ngumba na serikali inapanga kuongeza alama zaidi zikiwemo za macho na uso ambazo zilinaswa katika usajili wa Huduma Namba.

Ikizingatiwa kwamba, awamu ya kwanza ya usajili wa Huduma Namba iligharimu Sh10.6 bilioni, mpango mpya wa serikali wa kupatia kila Mkenya nambari ya kipekee ya kujitambulisha unakadiriwa kugharimu pesa zaidi.

“Tuko na mfumo wa kitambulisho ambao sio wa dijitali kamili. Kuendelea mbele, tutaimarisha mfumo wetu wa sasa wa kutambua vidole kuwa wa kibaiometriki ambao ni zaidi ya alama ya kidole na unahusisha alama za macho, alama za vidole na uso,” akasema Profesa Kindiki.

Katika kuendeleza ajenda ya serikali ya kukumbatia tekinolojia, Waziri Kindiki alisema kitambulisho kipya kitakuwa kikithibitishwa kupitia mtandao kwa kutumia nambari maalumu.

Waziri alieleza kuwa, watoto wapya wanaozaliwa Kenya watakuwa wa kwanza kusajiliwa katika mfumo mpya wa kufanya huduma zote za serikali kuwa za dijitali.

“Kuendelea mbele, tutakuwa na kitambulisho cha kitaifa kinachoweza kusomwa na mashine ya elektroniki na nambari maalumu na hatimaye, tutakuwa na mfumo wa kitambulisho wa dijitali ambao utakifanya kithibtishwe kupitia mtandao na nambari ya kipekee ya utambuzi ambayo tutapatia kila mtoto anayezaliwa Kenya na kufikisha umri wa miaka 18,” alieleza waziri Kindiki.

  • Tags

You can share this post!

Thamani ya Saka yapanda mara 5, sasa kutia mfukoni Sh2.5...

Hospitali ya watoto ya Gertrude’s yaahidi kuboresha...

T L