• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Jamaa wa Gumo aliyetekwa nyara aachiliwa

Jamaa wa Gumo aliyetekwa nyara aachiliwa

Na MARY WAMBUI

JAMAA wa waziri msaidizi wa zamani, Fred Gumo, aliyekuwa ametekwa nyara saa chache baada ya kumchukua mwanawe kutoka gereza la Kamiti ambapo alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 10 kwa kujihusisha na ugaidi, hatimaye aliachiliwa Jumamosi.

Bi Jacinta Bwire, shemeji wa Gumo, pamoja na dereva wake Willis Otieno, walitekwa nyara na watu wasiojulikana mnamo Ijumaa.

Bi Bwire na Bw Otieno waliachiliwa Jumamosi usiku na Jumapili mtawalia.

Elgiva Bwire Oliacha aliyetupwa jela kuhusiana na mashambulio mawili ya gruneti jijini Nairobi mnamo 2011, hakujulikana alikopelekwa na watekaji wake hadi wanaharakati walipolalamikia kutekwa kwao.

Wakili wake Prof Hassan Nandwa pia alitoweka muda mfupi baada ya kuripoti kutoweka kwa Bwire katika Kituo cha Polisi cha Central.

Bi Jacinta Bwire ni dada wa mmoja wa wake wa Bw Gumo na anafanya kazi katika serikali ya Kaunti ya Nairobi. Bw Gumo aliagiza dereva wake Bw Otieno, kumpeleka Bi Bwire katikati ya jiji la Nairobi kwa kutumia gari aina ya Landcruiser.

Lakini walipokuwa wakirejea nyumbani katika eneo la Karura jioni, waliandamwa na gari aina ya pick-up ambalo liliendeshwa kwa kasi na kuwafungia barabara karibu na lango kuu la kuingia nyumbani kwa Bw Gumo.

Wanaume watatu walitoka katika gari la pickup na kuagiza Bi Otieno na Bi Bwire kutoka ndani ya gari walilokuwa wameabiri.

Wawili hao walilazimishwa kuingia ndani ya gari hilo la pick-up na kuondoka nao.

Mnamo Jumapili, familia ilisema kuwa waathiriwa wanaendelea vyema bila kufichua mahali ambapo jamaa zao walizuiliwa tangu Ijumaa.

Elgiva, inadaiwa alinyakwa na watu waliokuwa na silaha, muda mfupi baada ya kufikishwa na mama yake katikati ya jiji la Nairobi kutoka Kamiti.

Mama yake alipofahamishwa kwamba mwanawe alitekwa nyara, alienda kumwambia Bw Gumo lakini yeye pia akatekwa siku hiyo.

Elgiva ambaye pia anajulikana kwa jina la Mohamed Seif, alifungwa baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki bunduki, risasi na gruneti bila leseni.

Mnamo 2005, Elgiva alijiunga na Uislamu kabla ya kuondoka nchini Kenya kuelekea nchini Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab.

Mnamo 2011, alirejea Kenya na kuishi mtaani Kayole ambapo alisajili vijana kadhaa kujiunga na kundi hilo la kigaidi.Baadaye mwaka huo, alikiri kuwa mwanachama wa al-Shabaab, kutekeleza mashambulio mawili ya kigaidi ambapo mtu mmoja aliuawa na 20 wakajeruhiwa na kujaribu kuingia uwanjani Nyayo na gruneti wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kenyatta, Oktoba 20 – ambayo sasa inajulikana kama Mashujaa.Kabla ya kukamatwa, mshukiwa pia alifichua kupitia Facebook kwamba alipanga kushambulia maeneo 13 jijini Nairobi kwa gruneti.

You can share this post!

Kaunti 43 hazijatengea ‘Big 4 Agenda’, ripoti yasema

Arudi na zawadi alipokosa mlo harusini

T L