• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Jamii ya Waboni yahofia mabilioni ya El-Nino yatawapita wakiwa msituni

Jamii ya Waboni yahofia mabilioni ya El-Nino yatawapita wakiwa msituni

NA KALUME KAZUNGU

JAMII ya Waboni wanaoishi vijiji vilivyoko ndani ya msitu mkuu wa Boni, Kaunti ya Lamu wanalia kutelekezwa na serikali kuu na kaunti kwenye mabilioni yanayotumika kukabiliana na janga la El-Nino nchini.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumanne, Novemba 28, 2023, Waboni wa vijiji vya Pandanguo, Jima, Milimani, Basuba, Bodhei, Mangai, Mararani na viunga vyake walisema licha ya kushuhudia wakazi wa vijiji vingine vya Lamu vilivyoathiriwa na mafuriko wakifikiwa na maafisa wa kaunti, serikali kuu na mashirika ya kusaidiwa kwa misaada msimu huu wa El-Nino, wao bado hawajafikiriwa na kufikiwa kusaidiwa kama wenzao.

Msemaji wa jamii ya walio wachache ya Waboni, Bw Ali Sharuti alisema tangu mvua kubwa ilipoanza kushuhudiwa, mahangaiko yamekithiri si haba vijijini kwani makazi yamekuwa hayakaliki tena ilhali njaa inawatafuna bila huruma.

Bw Sharuti aliomba hatua za haraka kuchukuliwa na misaada kufikishwa vijijini mwao ili na wao wajihisi kuwa Wakenya.

“Mashamba yetu yote yamejaa maji. Mimea imeharibika. Barabara yetu ya Pandanguo-Witu, ambayo ndiyo kiunganishi cha pekee kutoka hapa kuingia madukani mjini Witu imekatika na uchukuzi unesitishwa. Njaa inatutafuna hapa. Sielewi kwa nini serikali na mashirika hawajafika, hasa hivi vijiji vyetu vilivyoko ndani ya msitu wa Boni. Wanafika na kukomea tu maeneo ya mijini ilhali sisi tukiachwa kuteseka. Tumechoka kutelekezwa. Pia sisi nasi tunahitaji hayo mabilioni yanayosemekana kutolewa kusaidia kukabiliana na athari za El Nino,” akasema Bw Sharuti.

Bi Halima Musa, mkazi wa Bodhei alieleza kusikitishwa kwake na jinsi serikali mashirika yanavyoendeleza kimya wakati Waboni wa vijiji vya msituni wakiendelea kuathiriwa na mvua ya El-Nino.

Bi Musa anashikilia kuwa licha ya barabara za msitu wa Boni kuwa mbaya, ikizingatiwa kuwa Al-Shabaab wamekuwa wakilenga wapita njia kwa vilipuzi anatarajia kwamba wafikishiwe misaada kupitia njia ya ndege.

“Najua wanatelekeza eneo hili la msitu wa Boni, hasa hapa Bodhei na viunga vyake kwa madai ya utovu wa usalama unaochangiwa na Al-Shabaab. Kama wanaogopapa hizi barabara zetu, kwa nini hawatumii helikopta kutuletea misaada eneo hili. Mabilioni ya El-Nino yapo na hawana sababu ya kutotufikia,” akasema Bi Musa.

Chifu Mstaafu wa Lokesheni ya Basuba, Bw Yusuf Nuri alishangazwa na utelekezwaji unaoendelezwa, akidai kuwa kati ya zaidi ya vijiji vinane vya msituni Boni, ni kijiji kimoja pekee cha Kiangwe ambacho wakazi wamefikiwa na kusaidiwa msimu huu ambapo mvua kubwa inaendelea kunyesha na kuathiri maeneo mengi nchini, ikiwemo msitu wa Boni.

“Walifika tu Kiangwe kupeleka msaada. Kiangwe ni eneo ambalo linapakana na Bahari Hindi kwa hivyo liko nje kabisa ya msitu wa Boni. Kwa nini hawafiki huku ndani. Wanatarajia sisi wananchi maskini tutumie hela zetu kusafiri makumi ya kilomita kujichukulia misaada Kiangwe. Huo mchezo ukome. Twakubali hili ni eneo lenye changamoto tele, ikiwemo usalama na usafiri, hasa msimu huu wa El-Nino ambapo barabara nyingi zimesombwa na hazipitiki lakini hiyo si sababu ya Waboni kutelekezwa. Pia sisi ni raia Wakenya. Serikali ina hela na mbinu nyingi za kutufikishia misaada hapa. Twaomba tuzingatiwe,” akasema Bw Nuri.

Zaidi ya Waboni 3,000 wanaishi vijiji vya Pandanguo na Jima vilivyoko kaunti ndogo ya Lamu Magharibi ilhali wengine zaidi ya 4,000 wakiishi kwenye vijiji vya Basuba, Milimani, Bodhei, Mangai, Mararani na Kiangwe, kaunti ndogo ya Lamu Mashariki.

Karibu nusu ya Waboni hao kwa sasa wanahangaika kwa mafuriko huku wakihitaji misaada ya dharura, ikiwemo vyakula, mahali pa kula, vyandarua, dawa na kadhalika.

  • Tags

You can share this post!

Anavyojitahidi kufufua mahindi ya rangi

Matineja wazazi wanusuriwa kutoka hali ngumu ya uchumi kwa...

T L