• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Wanaume wawili wauguza majeraha baada ya kushambuliwa na kiboko

Wanaume wawili wauguza majeraha baada ya kushambuliwa na kiboko

NA KALUME KAZUNGU

WATU wawili wanauguza majeraha mabaya ya mikono, mabega, mbavu na miguu baada ya kushambuliwa kwa kuumwa na kiboko aliyekuwa akirandaranda kwenye kijiji cha Mapenya, kaunti ya Lamu.

Wawili hao, Omar Kalume Kalama,35, na mwenzake, Anthony Ndonga,30, wamelazwa kwenye hospitali ya Mpeketoni wakipokea matibabu.

Akithibitisha kisa hicho Alhamisi, Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS), Kaunti ya Lamu, Ibrahim Ahmed, alisema maafisa wake tayari wamefika eneo la tukio na kumfurusha kiboko huyo kurudi kwenye makazi yake kule kwa bwawa Mkunumbi.

Bw Ahmed aliwasihi wananchi kupiga ripoti kwa KWS haraka iwezekanavyo iwapo watashuhudia wanyama pori hatari wakirandaranda ili wasaidiwe kufurushwa kutoka kwa makazi yao.

“Kuna watu wawili waliong’atwa na kiboko eneo la Mapenya karibu na Mkunumbi. Walifaulu kuponyoka. Kwa sasa wako hospitalini Mpeketoni wakiuguza majeraha. Maafisa wetu wamefika maeneo husika kumfurusha kiboko huyo. Ninawahimiza waathiriwa kujaza fomu maalum na kuziwasilisha kwa kamati husika ya fidia kwa waathiriwa wa wanyamapori eneo hili. Baadaye kesi zao zitatathminiwa na kuwasilishwa kwa ofisi kuu jijini Nairobi. Zikipasishwa watalipwa fidia,” akasema Bw Ahmed.

Visa vya migogoro kati ya wanyama pori na binadamu vimekithiri kwenye maeneo mengi ya Kaunti ya Lamu kutokana na kwamba sehemu hiyo ina utajiri mkubwa wa misitu, ikiwemo ule mkubwa wa Boni.

Wakulima, hasa wale wa vijiji vya Pandanguo, Mavuno, Poromoko, Juhudi, Nyatha, Salama, Widho, Maleli, Maisha Masha, Katsaka Kairu, Kakathe, Moa, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe na maeneo mengine wamekuwa wakikadiria hasara kila mara kutokana na uharibifu wa mimea unaoendelezwa na wanyamapori.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume ajichoma moto Loitoktok baada ya kukataliwa na...

Jeshi langu linawindwa, adai Raila kuhusu kukamatwa kwa...

T L