• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Jinamizi la ahadi Ruto akizuru Magharibi

Jinamizi la ahadi Ruto akizuru Magharibi

JUSTUS OCHIENG, JESSE CHENGE na WINNIE ONYANDO

RAIS William Ruto anatarajiwa kuanza rasmi ziara yake Magharibi mwa Kenya Agosti 27, 2023 huku jinamizi la ahadi likiwa linamkodolea macho.

Ziara hiyo inatarajiwa kuwa italeta maendeleo kadhaa katika eneo la Magharibi.

Tayari Mbunge wa Bumula Jack Wamboka mapema wiki hii alitoa onyo kwa Rais Ruto kwamba jamii ya Mulembe itasubiri kuona kama atawaandalia mapochopocho kama alivyofanya alipokuwa ziarani Mlima Kenya wiki chache zilizopita.

“[Ruto] Aje na kiwanda cha sukari alichoahidi wakati wa kampeni,” ananukuliwa kwenye video iliyoambatishwa kwenye taarifa hii.

 

Jumapili, Rais Ruto atakuwa Kaunti ya Busia na Jumatatu atakuwa Bungoma kisha kuelekea Kaunti za Kakamega na Vihiga.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi katika eneo hilo tayari wanamtaka rais atoe ufafanuzi wa wazi kuhusu msimamo wa serikali yake kwa jamii ya Mulembe.

Hii ni kutokana na makubaliano ya awali ya kabla ya uchaguzi wa Agosti ambapo Dkt Ruto aliahidi kutengea mkoa huo asilimia 30 ya serikali yake na hata kuahidi kujenga angalau kilomita 1,000 za barabara.

Katika mapatano ya kabla ya uchaguzi na vyama vya Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya, rais Ruto, ambaye wakati huo alikuwa Naibu Rais, aliahidi kumpa Bw Mudavadi wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri huku Bw Wetangula kupewa nafasi ya Spika wa Bunge wa kitaifa, ahadi aliyotimiza.

Jana, kamati inayosimamia maandalizi ya ziara hiyo iliambia Taifa Leo kwamba eneo hilo liko tayari kumpokea Rais Ruto.

Naibu Gavana wa Kakamega, Ayub Savula, alisema Bw Mudavadi kama afisa mkuu kutoka eneo hilo ndiye atasimamia ziara hiyo huku Bw Wetang’ula akitarajiwa kuwaongoza wabunge.

Naye Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA), Cleophas Malal, alisema rais amejitolea kuzuru mkoa huo ili kuleta maendeleo na kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali inatekelezwa na pia kufufua viwanda vilivyoporomoka.

Aliwaongoza baadhi ya viongozi kutoka kaunti tano za Kakamega, Vihiga, Bungoma, Trans Nzoia na Busia Ikuluni ambapo walijadili masuala mbalimbali yatakayowasilishwa kwa rais.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi aitaka KRA iibuke na mbinu bora za ukusanyaji...

Chomelea ashtakiwa kwa kumpachika tineja mimba

T L