• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Jinsi ya kukwepa wahalifu unapomumunya Krismasi

Jinsi ya kukwepa wahalifu unapomumunya Krismasi

NA WACHIRA ELISHAPAN 

Msimu wa Krismasi huwa na mahanjamu na vituko tele ambavyo vyote hufanywa kwa kusudi la kupata raha. Ni kawaida kumpata mtu asiyeonja pombe maishani mwake akipiga funda la pombe kwa wakatii huo tu.

Watu wanapoamua kuponda raha, Mara nyingi huwa wamekondolewa macho na mambo mengi yanayohatarisha maisha yao. Nao wahalifu wanapata mwanya kuvuna wasipopanda.

Ili kuepuka wahalifu hao,ni vyema unapoamua kwenda kusharabia kileo chako,hakikisha kwamba umetenga na kubeba pesa mahsusi kwa vileo pekee.

Hili litakusaidia kuepuka kutumia pesa ovyo bila utaratibu wote. Kuko huko kwenye baa,wapo watu ambao wanangoja ushindwe kujidhibiti vizuri,ili wakusaidie huku wakikupora chochote ulicho nacho mfukoni.

Aidha, ni haki iwapo lazima unywe pombe,kunywa pombe kiasi utakachoweza kujidhibiti na ambacho hakitavuruga fikra na urazini wako. Baadhi ya wahalifu huja kwenye maeneo unayopenda ili kukukanganya na kuvuruga fikra zako ili kukuibia ulichojibakishia. Kumbuka kwamba baada ya kunywa pombe hiyo kuna namna ya kurejea nyumbani.

Kutobeba kadi yako ya kutoa pesa kutoka kwa banki ni njia nyingine ya kuepuka kukanganywa na wahalifu. Wahalifu wengi hii leo wanatumia teknolojia kuwaibia watu.

Baadhi ya watu wamekiri kupulizwa kemikali Fulani inayovuruga urazini wao,kisha wahalifu hao wanawaeleza kwenye banki au ATM kutoa pesa na kuwapa pesa hizo,kisha wakagundua kwamba wametapeliwa baadaye. Ili kuepuka hayo,iache kadi yako nyumbani kisha uwe na pesa taslimu za kutoshea matumizi ya wakati huo pekee.

Isitoshe usifungue bia yako ikiwa hutaimaliza kwani huenda ukaiacha mezani ikatiwa sumu. Wahalifu wengi huwaibia watu baada ya kuwasumu. Iwapo lazima utoke kabla ya kumaliza kileo chako,basi ondoka nacho ukienda uendako. Hii itakuepusha zani ya kuuliza aliyekutilia dawa. Badala yake, jijali kwa kufanya mambo yako kwa utaratibu.

Kadhalika,hakikisha hujakwenda popote pweke. Ni vyema unapotembea popote uhakikishe kwamba una rafiki ambaye unaweza kumtegemea na kumwamini. MTU kutoka familia yako angefaa zaidi kwani unamjua vyema na anakuamini. Msimu kama huu,watu wengi hujipata katika mikono mibaya ya marafiki wanaojifanya kuwajali ila linapowapata gumu wanatoweka.

Unaposherehekea Krismasi, kumbuka kwamba kuna kesho, na kesho inatanguliwa na leo. Jitenge na uhalifu kwa kuwa uhalifu ni hasara tupu.

You can share this post!

Wasichana wengi zaidi wakeketwa msimu wa Krismasi

Wakazi wa Nairobi walia Krismasi imekuwa ‘kavu’