• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Karua aipinga BBI akiwa katika ngome ya Raila

Karua aipinga BBI akiwa katika ngome ya Raila

Na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Narc Kenya Martha Karua, Jumapili alitofautiana na viongozi chama cha ODM kuhusu kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Viongozi hao waliohudhuria mazishi ya Angelina Kodiaga, mama ya mwanasiasa Profesa Israel Kodiaga yaliyofanyika Nyahera kaunti ya Kisumu, walitofautiana kuhusu iwapo katiba inafaa kubadilishwa wakati huu ambao kuna masuala muhimu yanayohitaji kushughulikiwa kwanza.

Bi Karua aliyeungana na mbunge wa Kisumu Magharibi Olago Aluoch, Spika wabunge la kaunti ya Kisumu Elisha Jack Oraro na mshirikishi wa BBI eneo la Nyanza Bob Madanje, alisema kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga hawatilii maanani maslahi ya Wakenya wengi.

“Nazungumza na kaka yangu mkubwa Raila na kaka yangu mdogo Uhuru, na swali ninalowauliza ni ikiwa wanasikiliza kilio cha Wakenya. Nimezuru maeneo yote Kenya na mimesikia manung’uniko kila mahali,” alisema Bi Karua.

Aliambia serikali ishughulikie masuala ya dharura kama ufufuzi wa uchumi baada ya corona na migomo ya wauguzi badala ya kampeni za refarenda.

Alisema kwamba katiba ya sasa inafaa kutekelezwa kikamilifu badala ya kufanyiwa mageuzi au wanaounga BBI wasikilize masuala ya wanaoipinga wanazua.

Kulingana na Bi Karua, Wakenya hawajapatiwa nakala za BBI wasome na kuielewa ilivyofanyika wakati wa kura za maamuzi za awali.

“Watu wanafaa kupigia kura kitu ambacho wamesoma na kuelewa na sio serikali kuambia watu wasome katika mtandao. Watu watanunua data au ni chakula cha kuwapa watoto wao,” alisema Bi Karua.

Pia, aliwaomba wanasiasa kuvumiliana na kuheshimiana wakati wa mdahalo kuhusu BBI na sio kuwazima wanaopinga mchakato huo.

“Tunapenda soka na lazima kuwe na timu mbili. Katika suala hili la BBI, nitakuwa katika timu inayosema la na nina sababu zangu,” alisema Bi Karua.

Mwanasiasa huyo pia alipinga kuongezwa kwa idadi ya maeneobunge.

Hata hivyo, Bw Madanje na Bw Oraro walisema kwamba baadhi ya viongozi wanaopinga BBI wanahadaa Wakenya.

“Kama washirikishi tunapanga mikutano itakayohudhuriwa na watu 200 kutoka kila kaunti ndogo. Wakati huo tutawapa nakala zilizorahisishwa ili mwananchi wa kawaida aweze kusoma na kuelewa,” alisema Bw Madanje.

Alisema mapendekezo ambayo hayakujumuishwa kwenye mswada wa BBI yatazingatiwa katiba itakapofanyiwa mageuzi siku zijazo.

Bw Oraro alisema BBI ina manufaa mengi kwa kuwa kaunti zitapata pesa zaidi na kutakuwa na hazina ya maendeleo katika kila wadi nchini.

You can share this post!

BI TAIFA JANUARI 4, 2021

Hatutaidhinisha ushindi wa Biden, maseneta 11 wasema