• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
Kaunti 4 eneo la Magharibi kupata chanjo mpya

Kaunti 4 eneo la Magharibi kupata chanjo mpya

Na CHARLES WASONGA

KAUNTI nne za magharibi mwa Kenya zinazokumbwa na uhaba wa chanjo dhidi ya corona zitapokea aina mpya ya chanjo kuanzia Jumatatu wiki ijayo.

Mwenyekiti wa Jopo kazi kuhusu utoaji chanjo hiyo Willis Akhwale jana alisema kaunti za Homa Bay, Migori, Bomet na Kericho zitasambaziwa chanjo aina ya Moderna iliyowasilishwa nchini wiki jana.

Mapema wiki hii, maafisa wa afya kutoka kaunti hizo walilalamikia kuwa wameishiwa na chanjo aina ya AstraZeneca kufuatia ongezeko la idadi ya watu wanaojitokeza kuchanjwa.

Kwa mfano Waziri wa Afya katika kaunti ya Homa Bay Richard Muga alisema wameishiwa na chanjo ilhali jumla watu 9,563 hawajapa dozi ya pili.

“Dozi ziliisha Ijumaa wiki jana wakati idadi kubwa ya watumishi wa umma na walimu walipewa chanjo,” akasema Profesa Muga.

Jana, Dkt Akhwale aliungama kuwa na habari kwamba kaunti nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo ya corona katika kaunti kadha.

“Ndio tuna habari kwamba kaunti hizo na nyingine zinakabiliwa na upungufu wa chanjo. Lakini tumeanza kusambaza chanjo aina ya Moderna na kuanzia Jumatatu zitaanza kuwasili katika kaunti hizo,” Dkt Akhwale akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Mnamo Jumatatu, Kenya ilipokea shehena ya dozi 880,460 za chanjo aina ya Moderna.

Chanjo hiyo ilitolewa kama msaada kutoka kwa Shirika la Kutoa Chanjo kwa mataifa yenye mapato ya chini (COVAX) na kusambazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu na Sayansi (UNICEF).

Shehena hiyo ilipokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na maafisa wa afya wakiongozwa Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi.

Dkt Akhwale, Ijumaa aliambia Taifa Leo kwamba usambazaji wa chanjo hiyo ulicheleweshwa kwa sababu maafisa wa kuchanja watu walihitaji kupewa mafunzo maalum.

“Kwa sababu hii ni chanjo spesheli, wahudumu wa afya walihitaji kupewa mafunzo maalum kabla ya kuanza kuwapa watu. Hii ndio maana tumechelewesha usambazaji wake,” akaeleza.

Dkt Akhwale aliongeza kuwa dozi milioni ya chanjo ya AstraZeneca pia itaanza kusambazwa kote nchini hivi karibu ili kupewa wale ambao wanasubiri dozi ya pili.

“Kwa hivyo, uhaba unaoshuhudiwa sasa ni wa muda tu, na utaisha hivi karibuni kwani serikali imejitoleaa kuhakikisha kuwa Wakenya wengi wanapata chanjo,” akasema.

Kulingana na Dkt Akhwale, uhaba wa dozi za chanjo ulichangiwa na onyo lililotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua kwa watumishi wa umma kwamba wale ambao hawajachanjwa wataadhibiwa.

“Matakaa ya Agosti 23 yaliyowekwa na Bw Kinyua ndio yalichangia wafanyakazi wa umma na walimu kujitokeza kwa wing. Kabla ya hapo kaunti kama vile Migori na Homa Bay zilirejesha dozi kadha baada ya muda wa matumizi,” akaeleza.

Dkt Akhwale aliongeza kuwa Kenya inatarajia kupokea jumla ya dozi milioni mbili za chanjo aina ya Pfizer kutoka nchini Amerika mwishoni mwa mwezi Septemba.

“Na kabla ya wakati huo, tutapokea shehena ya kwanza ya chanjo aina ya Johnson & Johnson yenye jumla ya dozi 390,000. Hii ni aina ya chanjo ambayo hutolewa kwa dozi moja pekee,” akasema.

Kufikia Ijumaa, watu 2,809,668 walikuwa wamepokea angala dozi ya kwanza ya chanjo dhidi ya corona.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Afya, watu 2,060,000 walikuwa wamepata dozi ya kwanza huku wengine zaidi ya 800,000 wakiwa wamepokea dozi ya pili.

You can share this post!

Msajili wa Vyama avunjilia mbali NASA

Agizo wanafunzi waliokosa kujiunga na sekondari wasakwe