• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Kawira roho mkononi akisulubiwa kwa mara ya pili Seneti

Kawira roho mkononi akisulubiwa kwa mara ya pili Seneti

NA MARY WANGARI

GAVANA wa Kaunti ya Meru, Kawira Mwangaza atajua hatima yake Jumatano Novemba 8, 2023 baada ya jopokazi maalum la Seneti linalosikiliza malalamishi dhidi yake kupiga kura ya kumdumisha au kumfurusha enzini.

Maseneta waliochaguliwa wasiopungua 24 watahitajika kupiga kura wakiunga mkono hoja iliyowasilishwa na Bunge la Kaunti ya Meru ili kuidhinisha pendekezo la kumng’oa afisini Gavana Mwangaza.

Jumla ya maseneta 47 wanatarajiwa kushiriki katika kura hiyo.

Mkuu huyo wa Kaunti anayewakilishwa na kikosi cha mawakili tisa anatazamiwa kusimama kizimbani hii leo ili kujitetea dhidi ya malalamishi yaliyowasilishwa dhidi yake na madiwani wa Bunge la Kaunti ya Meru kupitia mawakili wao wawili.

Aidha, mawakili wanaowakilisha madiwani wa Meru, Muthomi Thiankolu na Marias Maranya wanatazamiwa kuwahoji mashahidi watakaowasilishwa na Bi Mwangaza, kabla ya Seneti ikiongozwa na Spika Amason Kingi kutoa kauli ya mwisho na kupiga kura ya maamuzi.

Hii ni mara ya pili katika muda wa miezi 10 pekee ambapo Bunge la Kaunti ya Meru ‘limemburura’ Gavana Kawira hadi mbele ya Seneti likitaka afunganye virago.

Madiwani wa Meru kupitia mawakili wakuu Thiankolu na Maranya wamewasilisha malalamishi saba dhidi ya Bi Kawira yanayojumuisha kutoheshimu mahakama, kutoheshimu Bunge la Kaunti, usimamizi mbaya na ufujaji wa rasilimali za kaunti.

Aidha, anadaiwa kuwadunisha viongozi wenzake wakiongozwa na Naibu Gavana, kufanya teuzi pasipo kufuata taratibu za kisheria ikiwemo matumizi mabaya ya afisi, kuwaajiri kazi jamaa wa familia yake, na kuita barabara ya umma jina la mumewe kinyume na sheria.

Katika malalamishi mojawapo, Seneti ilielezwa jinsi Gavana Kawira alivyowapeleka dada, kaka na shemeji yake Urusi kama jopo la kiufundi kwenye ziara rasmi iliyokusudiwa kutathmini vifaa vya matibabu katika Kituo cha Saratani Kaunti ya Meru.

Miongoni mwa jamaa hao watatu, dada yake Bi Kawira aliye na stashahada katika taaluma ya dawa ndiye aliyekuwa na kiwango cha juu zaidi cha masomo.

Kupitia mawakili wao, madiwani jana waliirai Seneti kumtimua Gavana Kawira wakisema licha ya kunusurika mara ya kwanza, amezidi kuwa mkaidi hasa kupitia kauli kaende kaende anayopenda kutumia katika mikutano yake ya hadhara.

“Badala ya kuzingatia ushauri aliopewa na kuepuka masuala yaliyosababisha jaribio la kumtimua mara ya kwanza, Gavana alichukua msimamo wa ukaidi huku akitumia kauli ya kaende kaende, kabaki kabaki, kumaanisha ‘sijali, liwalo na liwe,” alihoji Wakili Mkuu Thiankolu.

“Kwa kuendelea katika ukaidi huo ni kama anaidhihaki Seneti akisema ‘oneni hata hamjui kuwafurusha watu afisini,” alisema wakili huyo akirejelea simulizi maarufu kutoka Urusi.

  • Tags

You can share this post!

Mwanadada kila akilala anaota jinsi ‘ex’...

Nahisi mwenzangu anapepeta ngoma kwa fujo!

T L