• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
KEBS sasa yasema unga wa Mokwa aliozindua Raila ni salama kwa lishe

KEBS sasa yasema unga wa Mokwa aliozindua Raila ni salama kwa lishe

GEORGE ODIWUOR na JUSTUS OCHIENG’

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) sasa linasema kuwa unga unaotengenezwa na Kiwanda cha Kusaga Mahindi cha Kigoto, Kaunti ya Homa Bay ni salama kwa matumizi.

Kebs imesema hivyo siku chache tu baada ya kusema unga kutoka kiwanda hicho ulikuwa na kiwango cha juu cha sumu ya aflatoxin (kuvu). Shirika hilo sasa linasema litaharibu shehena ambayo ina unga huo wenye sumu.

Mnamo Ijumaa Meneja wa Kebs ukanda wa Ziwa Viktoria Andrew Maiyo na Gavana Gladys Wanga waliandaa kikao na wanahabari ambapo walisema unga huo maarufu kama Mokwa (unga wetu) sasa ni salama kwa matumizi ya raia.

Ripoti ya Kebs mnamo Septemba 13, 2023 ilifichua kuwa sampuli za unga huo zilizopimwa mnamo Agosti 28 zilikosa kutimiza viwango vinavyohitajika vya Kebs. Ripoti hiyo ambayo ilitiwa saini na Menejea wa kieneo Bernard Sindani iliagiza unga ambao ulikuwa umetolewa sokoni, urejeshwe kiwandani.

Hii ni baada ya vipimo kwenye maabara kuonyesha kuwa unga huo ulikuwa na asilimia 19.46 ya aflatoxin dhidi ya kiwango kinachoruhusiwa kisichopita asilimia 10.

Bw Maiyo alisema kuwa wamebaini unga huo ambao ulizinduliwa rasmi na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga mnamo Novemba mwaka jana, sasa umetimiza viwango vyote vya kiusalama vinavyohitajika na Kebs.

Meneja huyo alisema kuwa waliwatuma afisa wao hadi Kigoto inayopatikana Suba na akafanya ukaguzi jinsi kiwanda hicho kinavyoendeleza shughuli zake ndipo akabaini kuwa unga ulikuwa na kiwango cha juu cha aflatoxin.

Hata hivyo, Bw Maiyo alisema si unga wote ulikuwa na kiwango cha juu cha sumu hiyo na baada ya tukio hilo wameidhinisha kiwanda hicho kiendelee na shughuli zake.

“Tungependa kuhakikishia umma kuwa Kebs ina mpango unaofuata kuhakikisha bidhaa zinazotolewa kwa umma ni salama mno. Kigoto ilitimiza viwango na masharti yote Novemba mwaka jana ndiposa tuliiruhusu isage unga,” akasema Bw Maiyo.

“Imeelezwa kuwa unga uliokuwa na sumu ulikuwa ukitumika kujaribu mashine mpya. Tutaharibu unga huo,” akaongeza.

Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi naye alitetea kiwanda hicho akisema huenda baadhi ya wafanyabiashara na wakulima waliwasilisha mahindi ambayo hayakuwa yamekauka vizuri.

“Tunatambua jukumu la Kebs la kuhakikisha kuwa bidhaa salama ndizo zipo sokoni. Inaonekana mahindi hayo hayakuwa yamekauka vizuri kutokana na wakulima wengi kukosa vifaa vya kuyakausha mahindi yao,” Bw Omondi akaeleza Taifa Leo.

Gavana Wanga alisema lengo la utawala wake ni kubuni nafasi za ajira na kiwanda hicho kitaendelea kutoa soko kwa wakulima.

“Tulihakikisha kiwanda kinapata cheti cha Kebs na shirika hilo limekuwa likifuatilia oparesheni zake kila mara. Tumechukua hatua ya kuharibu bandali 36 za unga ambazo zilikuwa zina viwango vya juu aflatoxin,” akasema Bi Wanga.

  • Tags

You can share this post!

Kamati yasema mfumo wa ukusanyaji mapato Nairobi...

Jengo la bodaboda mjini Kisii ni ‘eneo la...

T L