• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Kamati yasema mfumo wa ukusanyaji mapato Nairobi ‘umejaa ukora’

Kamati yasema mfumo wa ukusanyaji mapato Nairobi ‘umejaa ukora’

NA WINNIE ONYANDO

KAMATI ya Bunge la Nairobi inayosimamia masuala ya teknolojia na mawasiliano ina wasiwasi kwamba hakuna uwazi na uwajibikaji katika mfumo wa ukusanyaji mapato jijini.

Kamati hiyo ililalamika kuwa serikali ya Gavana Johnson Sakaja haina mfumo bora wa kukusanya mapato.

“Ni wazi kuwa kaunti imekosa mfumo halisi wa kuonyesha jinsi mapato ya Kaunti ya Nairobi yanavyokusanywa, kuripotiwa na kuhesabiwa,” akasema diwani wa Kileleshwa Robert Alai katika ukumbi wa City Hall mnamo Ijumaa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kuiorodhesha Nairobi kuwa ni mojawapo ya kaunti ambazo zimekosa uwajibikaji katika mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

Diwani Alai alibainisha kwamba Idara inayosimamia Fedha katika Ofisi ya Gavana haina fununu wala ufahamu wa jinsi ukusanyaji wa mapato unavyosimamiwa Nairobi.

“Wizara ya fedha kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi haina ufahamu kuhusu yanayoendelea. Hii ndiyo maana tunasema kuna haja hatua ya haraka ichukuliwe,” akaongeza Bw Alai.

Kando na hayo, kamati hiyo ilisema kuwa wizara ya sasa na ile ya awali hazina ufahamu kuhusu anayesimamia mfumo wa kukusanya mapato.

Kamati hiyo pia ilidai kuwa bunge hilo halijabainisha ni akaunti ngapi za benki zinazohusishwa na mfumo wa kukusanya mapato.

Hata hivyo, Gavana Sakaja alisema kuwa serikali yake imekumbatia mfumo wa kidijitali kukusanya mapato.

  • Tags

You can share this post!

Gaspo Women walenga kuharibu mwanzo mzuri wa Vihiga Queens

KEBS sasa yasema unga wa Mokwa aliozindua Raila ni salama...

T L