• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Kemsa kuteketeza dawa za Sh1.8 bilioni zilizoharibika

Kemsa kuteketeza dawa za Sh1.8 bilioni zilizoharibika

Na ANTHONY KITIMO

Mamlaka ya Kusambaza Dawa Nchini (KEMSA) imesema kuwa itaharibu dawa ambazo muda wao wa matumizi umepitwa na wakati na vifaa, zote ambazo zina thamani ya zaidi ya Sh1.8 bilioni.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, baadhi ya dawa hizo zililetwa na wafadhili na hazikusambazwa kwa makundi na hospitali ambazo zilikuwa zikilengwa kwa wakati.

Mwenyekiti wa Kemsa Irungu Nyakera alisema mamlaka hiyo imepata idhini ya Baraza la Mawaziri ili kuharibu shehena hizo ambazo zipo kwenye hifadhi mbalimbali nchini.

“Katika mwaka uliopita wa fedha, tulikuwa na shehena kubwa ambayo inastahili kuharibiwa na thamani yake ni zaidi ya Sh1.8 bilioni. Dawa hizo zililetwa na mfadhili na kulikuwa na mawasiliano ya kuchelewa kuhusu mahali ambapo zingepelekwa. Nyingine zilistahili kutumika wakati ambapo ziliwasilishwa na sasa zimepitwa na wakati.” akasema Bw Nyakera.

“Shehena kubwa ambayo itaharibiwa ina dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi. Hata hivyo, dawa hizo sasa haziwezi kutumika kwa kuwa nyingine ziliwasilishwa,” akaongeza Bw Nyakera.

Kulingana na Kemsa, dawa huharibiwa iwapo haziwezi kutumika kwa jukumu lengwa hasa baada ya bakteria kukua na kuenea kiasi cha kutoweza kufa kutokana na makali ya dawa zenyewe.

Akizumgumza akiwa Mombasa kwenye kikao na wanahabari, Bw Nyakera alisema Kemsa inafanya kazi kuhakikisha kuwa dawa zinazowasilishwa kwa kaunti zote 47 zinaongezwa. Hii ni kati ya mikakati ya kuzuia hali ambapo uhaba wa dawa hushuhudiwa kwenye hospitali na baadhi ya vituo vya afya.

“Tangu kuanza kwa mwaka huu wa fedha, tumepokea ombi kutoka kwa kaunti 38 hadi 48 na tunatumai kuwa huduma itaimarika baada ya kuwasilishwa kwa dawa hizo,” akasema Bw Nyakera.

Mwenyekiti huyo alifichua kuwa Kemsa inazidai kaunti Sh2.9 bilioni kutokana na dawa zilizowasilishwa siku za nyuma ila inafanya kazi karibu na Baraza la Magavana Nchini (COG) na serikali za kaunti ili kupata pesa hizo.

“Tunawasilisha dawa na vifaa vingine vya kimatibabu kwenye zaidi ya vituo 98,100 kote nchini kwa deni kisha sisi hulipwa baadaye. Kile tunaomba kaunti ziongeze ni hifadhi za dawa kwa asilimia 80 ili kupunguza uhaba unaoshuhudiwa,” akasema Nyakera.

“Pia tumeweka mikakati kuhakikisha kuwa dawa zinazosambazwa na serikali hazifiki kwenye vituo vya afya vya watu binafsi. Tunahakikisha hii inatimia kwa kuweka alama kwenye muhuri,” akasema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Afya kwenye Baraza la Magavana Nchini (COG) Muthomi Njuki alizitaka kaunti ambazo zimesalia na bado hazizingatii kanuni za Kemsa, zitume mawasiliano ili kupata dawa zao.

“Hapo awali tulikuwa na masuala mbalimbali na Kemsa ila tunashauriana na serikali za kaunti ili zipate dawa zao kwa wakati. Kuzipa kaunti jukumu la kusambaza dawa kumesababisha hospitali mbalimbali kukumbwa na uhaba,” akasema Bw Njuki.

  • Tags

You can share this post!

Mpinzani jela miaka 7 kwa ‘kumtusi’ Rais Tshisekedi

Mshambulizi Judith Atieno arefusha mkataba klabuni Rayon...

T L