• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Kiini cha wavulana kutorejea shuleni

Kiini cha wavulana kutorejea shuleni

Na WAANDISHI WETU

WAVULANA wengi kote nchini, wameshindwa kurudi shuleni kwa kuwa walizoea kupata pesa wakiwa nyumbani shule zilipofungwa kwa sababu ya janga la corona na kushiriki desturi za jamii zao.

Baadhi yao wanashiriki matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu.Wengi wao wamezoea kufanya kazi ya bodaboda ambayo imekuwa vigumu kuacha kwa kuwa wanapata pesa.Katika shule za eneo la Rift Valley, idadi ya wavulana ambao hawajarudi shule inapiku ile ya wasichana.

Wengine walishirikishwa katika tohara na kujiunga na Wamoran, wizi wa mifugo, kufanya kazi katika timbo za mawe na uchuuzi wanakopata pesa.

Katika kaunti ya Samburu, maafisa wanasema kwamba wavulana 30,000 hawajarudi shuleni baada ya kuwa Moran.

“Twakwimu zetu zinaonyesha kuwa tumepoteza wavulana wengi kuliko wasichana. Tuna wasiwasi ikizingatiwa idadi ya wavulana walioripoti shuleni kote katika kaunti,” alisema mkurugenzi wa elimu wa kaunti ya Samburu David Koech.

Katika kaunti ya Nyandarua, wavulana wanaofaa kuwa shuleni wanafanya kazi ya bodaboda sehemu za mijini wakiwakwepa maafisa wa usalama.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa katika kaunti za Kajiado, Kericho, Laikipia, Samburu na Baringo baadhi ya wavulana waliopashwa tohara hawakurudi shuleni.

Mwenyekiti wa chama cha wanabodaboda mjini Kitengela, kaunti ya Kajiado, Bw Daniel Muiruri alisema kuwa wanakagua waendeshaji wote ili kuwatambua wanafunzi.

Wanafunzi hao wamekuwa wakikodisha pikipiki kwa kati ya Sh300 na Sh500 kwa siku. Mwenyekiti wa chama cha wanabodaboda kaunti ya Kajiado Alex Gitari alisema kuna zaidi ya wanafunzi 500 wanaoshiriki biashara ya bodaboda katika kaunti hiyo.

Mwenyekiti wa chama cha wazazi kaunti ya Isiolo Ismael Galma alisema kwamba wavulana wengi hawajaripoti shuleni hasa katika kaunti ndogo ya Isiolo kwa sababu ya kutekwa na uraibu wa dawa za kulevya.

Katika kaunti ya Nairobi, mwanafunzi wa kidato cha tatu alishtakiwa kwa kuongoza genge la majambazi kumnyang’anya mtu simu na Sh6,000 na kumjeruhi kwa kumpiga risasi.

Hakimu Mkuu Mkazi Philip Mutua aliagiza umri wa mwanafunzi huyo uthibitishwe kabla ya kumwachilia kwa dhamana.Katika kaunti ya Lamu, viongozi na wazee, wameelezea kutamaushwa kwao na ongezeko la vijana wanaotumia dawa za kulevya eneo hilo. Wakizungumza na wanahabari, viongozi hao, akiwemo mbunge wa Lamu Mashariki,

Athman Sharif na mbunge Mwakilishi wa Wanawake eneo hilo, Bi Ruweida Obbo walisema hawajafurahishwa na jinsi vijana wengi kote Lamu wanavyoendelea kutumia mihadarati.Bw Sharif alieleza haja ya idara ya usalama eneo hilo kuwasaka na kuwachukulia hatua kali za kisheria wasambazaji wa mihadarati ili wasiendelee kuharibu maisha ya vijana.

Ripoti za Waweru Wairimu, Stanley Ngotho, Joseph Ndunda, Kalume Kazungu, Geoffrey Ondieki na Flora Koech.

You can share this post!

Fowadi matata Onyango atupwa nje ya timu ya taifa ya hoki

Ruto na Raila wazidi kuraruana kuhusu utawala wa Jubilee