• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 11:13 AM
Kiraitu akerwa na matamshi ya Ruto

Kiraitu akerwa na matamshi ya Ruto

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Meru Kiraitu sasa amejibu Naibu Rais William Ruto ambaye alimshutumu juzi kwa madai kuwa anaunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais, 2022.

Katika ujumbe kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Bw Murungi aliyataja madai ya Dkt Ruto kama siasa za chuki na ambazo hazina msingi wowote.

“Watu wa Meru wanataka kusikia sera za kuimarisha kilimo cha miraa, majani chai, kahawa, uzalishaji maziwa na vitega uchumi vingine wala sio matusi ambayo hayana manufaa yoyote kwao,” akasema.

“Usije kwetu Meru kudai kuwa ni wewe pekee unayestahili kuungwa mkono na kwamba ni hujuma kwetu kukaribisha wagombeaji urais wengine Meru. Tangu lini Meru iligeuka kuwa mali yako. Meru ni yetu,” Gavana Murungi akaongeza.

Kiongozi huyo alisema kuwa wakazi wa Meru wako huru kuwasikiliza wagombeaji wengine wa urais kabla ya kufanya uamuzi wao wa mwisho.

Gavana Murungi alimtaka Dkt Ruto kuomba kura za Wameru kwa upole na unyenyekevu bila kuwalazimisha au kuwashurutisha.

Wakati wa ziara yake ya kampeni ya siku mbili katika Kaunti ya Meru kuanzia Jumapili, Naibu Rais alimwonya Gavana Murungi dhidi ya kile alichotaja kama kuwalazimisha wakazi kumuunga mkono Bw Odinga.

You can share this post!

Huenda ahadi za wanasiasa ni maneno matamu tu

Mahakama yakubali ushindi wa marehemu Jeniffer Wambua...

T L