• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Korti yaamua aliyemuosha Mungatana Sh76m ana kesi ya kujibu

Korti yaamua aliyemuosha Mungatana Sh76m ana kesi ya kujibu

NA RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Chad anayedaiwa alimlaghai Seneta wa Tana River Danson Mungatana kitita cha Sh76 milioni akitumia nguvu za ndumba huku akidai ataziongeza maradufu, amepatikana ana kesi ya kujibu.

Baada ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi kufikia uamuzi huo, alimwagiza mshukiwa, Abdoulaye Tamba Kouro, aanze kujitetea Septemba 21, 2023.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote, hii mahakama imefikia uamuzi kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuwezesha mshtakiwa kuwekwa kizimbani kujitetea,” aliagiza Bw Ekhubi.

Bw Ekhubi alifikia uamuzi wa kumweka Kouro kizimbani baada ya kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki kwamba “upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kumsukuma mshtakiwa kizimbani kujitetea.”

Bi Kariuki alieleza hakimu ushahidi uliowasilishwa utathibitisha kwamba Kouro alimdanganya Bw Mungatana atazifanya maradufu pesa atakazowekeza.

Bw Mungatana alipotoa ushahidi kortini, alisema alianza kumpa mshtakiwa idadi ndogo ya pesa alizozifanya kuongezeka maradufu.

Alianza kwa kumpa Sh1 milioni akarudishiwa Sh2 milioni.

Seneta huyo alieleza mahakama kuwa alimpa tena Sh5milioni zikafanyiwa kuongezeka zikawa Sh10 milioni.

Lakini baadaye alipompa Kouro dola milioni moja (Sh76milioni za wakati huo) alizima simu na kutoweka.

Seneta huyo alisema mshtakiwa alisakwa kwa udi na uvumba hadi pale alipokamatwa na maafisa wa polisi wa kikosi kilichovunjwa cha Flying Squad.

Kouro anakabiliwa na mashtaka ya kumlaghai Bw Muungatana Sh76 milioni kati ya Aprili 20, 2011 na Aprili 29, 2013 katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.

Mbali na Bw Mungatana, Kouro pia ameshtakiwa kwa kumlaghai Makau Muteke dola 6,796 akidai atamuekezea hadi zimpe faida maradufu.

Bw Mungatana aliambia mahakama aliamua kujitokeza hadharani kwa vile karibu ulaghai huo umsukume katika hali ya uchochole.

Pia Kouro alishtakiwa kupatikana na pesa feki za kigeni sawa na Sh960,120,000 zilizojumuisha Dola za Marekeni na sarafu za Euro.

Bw Mungatana alileza mahakama kuna mabwanyenye wengi walioporwa na mshtakiwa lakini waliona aibu kujitokeza wasiaibike na kufedheheka.

Pia Bw Mungatana alisema ilibidi auze jumba lake la kifahari mtaani Karen na hata mkewe hakumwamini ameuza jumba hilo ila alifikiria mtu mwingine alikuwa akiishi mle.

Aliambia korti aliuza magari yote aliyokuwa ameandikisha kwa jina la mkewe ambaye baadaye alifariki.

Bw Mungatana aliomba hakimu amsukumie kifungo cha muda mrefu mshtakiwa kwa vile amewasababishia Wakenya wengi dhiki.

  • Tags

You can share this post!

Wito mashamba makubwa ya kilimo yalindwe kazi zisipotee

Al-Shabaab: Wakazi wafanya maandamano kuitaka serikali...

T L