• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Wito mashamba makubwa ya kilimo yalindwe kazi zisipotee

Wito mashamba makubwa ya kilimo yalindwe kazi zisipotee

NA LAWRENCE ONGARO

MKURUGENZI wa kampuni ya Delmonte anayeondoka Bw Stregios Gkaliamoutsas, amesema kuna haja ya mashamba makubwa ya kilimo kulindwa ili yasinyakuliwe na kutumika na watu wenye ubinafsi wasiotaka vijana na vibarua kuwa na ajira.

Alitoa mfano kwamba kando ya barabara kuu ya Thika Superhighway, kuna mashamba makubwa mengi ambayo yanatumika kama maeneo ya ujenzi wa majumba tu, tofauti na awali ambapo yalikuwa ya kilimo.

“Mashamba ya kilimo yana umuhimu wake kwa sababu wafanyakazi wengi wanapata ajira za shambani. Isitoshe, husaidia kuimarisha uchumi wa nchi,” alisema mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo alisema kwa muda wote ambao amekuwa nchini kwa miaka 24, kampuni imejitahidi kuhakikisha mashamba yanalindwa kwa minajili ya kilimo cha matunda ya mananasi.

Kulingana na mipango iliyopo, tayari kampuni ya Delmonte imeipa kaunti ya Murang’a kiasi cha ekari 1,400 huku nayo kaunti ya Kiambu ikipata ekari 700.

Lakini katibu wa muungano wa wafanyakazi wa Food and Allied Workers Union Bw Boniface Kavuvi, alipinga hatua hiyo ya kampuni hiyo kuachilia mashamba hayo, akidai ya kwamba wafanyakazi wengi watakosa ajira, haswa waliokuwa wakifanya kazi zao katika mashamba hayo makubwa ya Delmonte.

“Sisi tunapinga hatua hiyo ya mashamba hayo kukabidhiwa kwa kaunti hizo kwa ujenzi wa majumba,” alisema Bw Kavuvi.

Alisema kampuni ya Delmonte inastahili kulinda mashamba yake ili yasije yakapungua siku zijazo.

Kampuni ya Delmonte ni miongoni mwa kampuni kubwa duniani na inaletea nchi hii mabilioni ya fedha za kigeni,” alisema katibu huyo.

Viongozi wengine wa chama cha mashambani cha wafanyakazi Bw Thomas Kipkemboi ambaye ni naibu katibu mkuu wa kitaifa na mwenzake Edwin Adala walisema watazidi kutetea wafanyakazi wao ili wasifutwe kazi sababu kuu ikiwa ni mashamba kuhamishiwa umiliki hadi kwingineko.

  • Tags

You can share this post!

Kikosi spesheli kutumwa Tana River na Lamu

Korti yaamua aliyemuosha Mungatana Sh76m ana kesi ya kujibu

T L