• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
KQ yaongeza Sh25 milioni kwenye Safari Rally

KQ yaongeza Sh25 milioni kwenye Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

KAMPUNI ya ndege ya Kenya Airways (KQ) imeongeza Sh25 milioni kwenye Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally zitakazoifanya kuwa mdhamini rasmi wa kutoa huduma za ndege.

Mnamo Juni 10, KQ ilitangaza kudhamini Wakenya chipukizi McRae Kimathi (26), Hamza Anwar (22) na Jeremy Wahome (22) kwa Sh10 milioni kuingia katika mradi wa kukuzwa na Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA).

Katika mpango wote wa KQ wa Sh35 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu, Sh25 milioni zitasaidia mbio zenyewe za Safari Rally, huku Sh10 milioni zikielekezwa kukuza madereva hao chipukizi mwaka 2021.

“Kupitia udhamini huu, timu yetu ya WRC Safari Rally Kenya pamoja na madereva hao chipukizi watapewa tiketi za ndege kuhudhuria mikutano na mashindano ya WRC kote ulimwenguni,” alitanguliza Afisa Mkuu Mtendaji wa KQ, Allan Kilavuka hapo Juni 20.

Aliongeza, “Pia, watanadi WRC kupitia jarida letu la Msafiri na matangazo mengine pamoja na burudani. Kusaidia shughuli muhimu kama WRC Safari Rally hakutainua tu moyo wa Ukenya, bali pia kutusaidia katika kunadi Kenya dunia nzima.

Sisi kama kampuni ya ndege ya taifa ya Kenya iliyo na jina na bendera ya taifa hili tunahisi kuwa uhusiano wetu na shughuli kama hii unafaa sana.”Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Michezo Amina Mohamed na Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya Safari Rally, Phineas Kimathi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mbio za Magari Kenya (KMSF), miongoni mwa wengine.

Amina alisifu ushirikiano kati ya serikali na kampuni za kibinafsi katika mbio za Safari Rally. Alisema zimesaidia sana katika maandalizi ya duru hiyo ya sita ya WRC itakayonufaisha sekta mbalimbali. Safari Rally itafanyika Juni 24-27 katika kaunti za Nairobi, Kiambu na Nakuru itakayoandaa sehemu kubwa ya mashindano hayo katika maeneo ya Naivasha.

  • Tags

You can share this post!

NAPSA Stars wanayochezea Wakenya Calabar na Odhoji yalemewa...

Penye nia pana njia