• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:31 PM
Penye nia pana njia

Penye nia pana njia

Na JOHN KIMWERE

WAHENGA waliposema penye nia pana njia hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa, maana ndivyo ilivyo tangia zama hizo na ipo hivyo mpaka sasa.

Usemi huo umeonesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii. Aidha ni msemo unaozidi kudhihirishwa na wengi ambao wameamua kujituma kisabuni huku wakiamini wanaweza kusudi watimize azma yao maishani.Patriciah Lihanda Indogo ni kati ya waigizaji wa kike humu nchini wanaolenga kufanya makubwa miaka ijayo.

Binti huyu anayekaribia kutinga umri wa miaka 24 ni mwigizaji anayekuja, mwana mitindo ‘Plus size,’ na msomi wa mwaka wa nne kwenye chuo cha Pioneer International anakosomea masuala ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu amani na ulinzi.

Kisura huyu amejiunga na uigizaji mapema mwaka huu baada ya kuvutiwa na maigizo tangia akisoma shule ya Msingi alipotazama kipindi cha Tahidi High ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Mali ya serikali ni tamu

Msichana huyu ambaye hufanya kazi na kundi la Nairobi Chronicles anajivunia kushiriki filamu fupi nyinyi tu ambazo hupeperushwa kupitia mtandao wa Youtube. Ameshiriki filamu kama ‘Ukienda kuona babymama na hakutaki,’ ‘Mali ya serikali ni tamu,’ na ‘Wanaume wamekaliwa chapati Nairobi’ kati ya zinginezo.

”Ndio nimeanza kupiga ngoma lakini baada ya miaka mitano ijayo nimepania kuwa katika kiwango cha juu hasa kushiriki filamu za kimataifa, Hollywood,” anasema na kuongeza kuwa anaamini ametunukiwa kipaji cha kufanya kweli katika tasnia ya maigizo.

 Picha/JOHN KIMWERE
Mwigizaji chipukizi Patriciah Lihanda Indogo

Katika mpango mzima analenga kufuata nyayo zake mwigizaji mahiri duniani Tiffany Haddish mzawa wa Marekani aliyeshiriki filamu kama ‘Night School,’ na ‘Nobodys fool,’ kati ya zingine.Anafichua kuwa tangia akiwa mtoto alidhamiria kuwa rubani au mwanamuziki maana aliwahi kununuliwa vyombo vya kujifunza masuala ya muziki lakini roho imekwenda kwingine.

Genivieve Nnaji

Anasema hapa nchini angependa kufanya kazi na waigizaji kama Sarah Hassan maarufu Tanya aliyeigiza kipindi cha Tahidi High na Saints (Citizen TV).Pia angependa kufanya kazi na mwezie Brenda Wairimu anayejivunia kushiriki filamu kama ‘Mali,’ na ‘Disconnect.

‘ ”Barani Afrika itakuwa furaha kubwa kujikuta jukwaa moja na waigizaji mahiri wa filamu za Kinigeria (Nollywood) kama Ini Edo na Genivieve Nnaji,” akasema. Edo na Nnaji wameshiriki filamu kama ‘Chief Daddy’ ‘Palace Maid,’ na ‘Blood Sisters,’ ‘Lionheart’ kati ya zingine. Anatoa wito kwa serikali iongezee majukwaa kama Viusasa ili wasanii kupata kuonesha uwezo wa talanta zao.

Changamoto

Anasema mwanzo alipoanza kushiriki uigizaji alijikuta kwenye wakati mgumu hasa kugawanya na shughuli za kuendeleza masomo yake. ”Haikuwa rahisi kufanya sote mbili lakini kwa sasa nimejifunza mengi na kufaulu kugawanywa muda vizuri,” akasema.

Anatoa wito kwa wasanii wenzie watie bidii wala wasiwe na pupa ya kufaulu upesi kila jambo huchukua muda pia anawaambia kuwa sekta ya uigizaji inahitaji ubunifu zaidi.

 Picha/JOHN KIMWERE

  • Tags

You can share this post!

KQ yaongeza Sh25 milioni kwenye Safari Rally

Chipukizi wa AFC Leopards Youth wazidi kutamba Ligini