• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kundi la Kwanza: Wakenya 227 waenda kutekeleza ibada ya Hajj mjini Mecca

Kundi la Kwanza: Wakenya 227 waenda kutekeleza ibada ya Hajj mjini Mecca

NA CECIL ODONGO

HUSSEIN Hassan Daban,72, na Mohamud Hassan Daban,66, wamejawa na tabasamu wakisubiri kuabiri ndege ya shirika Kenya Airways kusafiri hadi nchini Saudi Arabia.

Kaka hao wawili ni miongoni mwa mahujaji 227 ambao Ijumaa walisafiri ili kutimiza mojawapo ya nguzo kuu za Uislamu ambayo niibada ya Hajj mjini Mecca nchini Saudi Arabia. Hajj au Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu. Mwislamu hutakiwa kuhiji angaa mara moja maishani mwake ikiwa ana uwezo.

Nguzu ya kwanza ni Shahada, ya pili ni Swala, ya tatu ni kutoa Zaka nayo ya nne ni kutii na kutekeleza ibada ya mfungo wa Saumu.

Licha ya umri kusonga sana, Daban anayeishi katika Kaunti ya Mandera na akishikwa mkono na mwanawe Bashir Hussein Hassan mara kwa mara, alionekana na bashasha usoni alipokuwa akisubiri kuabiri ndege.

“Nina furaha wakati huu nikitaka kuenda Mecca kwa ibada ya Hajj na ninaomba Allah akubali maombi yangu. Mwaka 2020 nilikuwa nimejiandaa vilivyo lakini janga la Covid-19 likavuruga kila kitu,” akasema Daban kwa lugha ya Kisomali huku mwanawe akitafsiri kwenye mahojiano na Taifa Leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.

Naye ndugu yake Mohamud anayeishi katika Kaunti ya Isiolo anasema kubwa zaidi atakalohakikisha ni kuhakikisha anatekeleza ibada kwa uadilifu na unyenyekevu mkuu asamehewe dhambi na arudi akiwa safi kwa maswala ya imani ya kidini. Anasema atarudi na maji ya Zamzam.

“Ni matarajio yangu kwamba nitarudi nyumbani na maji ya Zamzam,” akasema Mohamud.

Naye Abdullahi Haji, 55, hii haikuwa mara yake ya kwanza kwenda kuhiji. Ni mara yake ya 13 na anasema afya ikimruhusu ataendelea kuhiji bora tu Mungu amemjalia uwezo wa kumudu gharama za Hajj. Mwaka huu 2023 atagharimika Dola 7000 (Sh980,000) ili kuhiji.

“Nilisomea nchini Saudi Arabia na pengine ndiyo sababu ambayo imefanya pia niende Hajj mara nyingi. Kwa mujibu wa dini, ukishiriki hafla na ibada takatifu unarudi ukiwa safi bila madhambi kama mtoto ambaye amezaliwa,” akasema Haji.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale,  viongozi wa Supkem wakiongozwa na Mwenyekiti Hassan Ole Naado na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Airways (KQ) Allan Kilavuka walikuwa hapo kuwatakia safari njema mahujaji.

Waziri Duale alisema serikali inafuatilia kuhakikisha Wakenya wanahiji bila matatizo yoyote.

“Tunatumai mtaomba amani ipatikane nchini na vile vile mvua inyeshe kwa sababu tumeshuhudia kiangazi. Serikali ya Kenya na ile ya Saudi Arabia zitashirikiana vilivyo,” akasema waziri Duale.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale awatakia safari njema mahujaji kutoka Kenya wanaoenda Mecca, Saudia Arabia kutekeleza ibada ya Hajj. PICHA | WILFRED NYANGARESI

Naye Bw Ole Naado amepongeza serikali ya Kenya na ile ya Saudi Arabia kwa kusaidia pakubwa wakati wa maanfdalizi ya safari hiyo ya mahujaji huku akieleza kwamba jumla ya Wakenya 4,000 watasafiri hadi mjini Mecca kufikia Juni 22 ambapo kundi la mwisho mwaka huu 2023 litakuwa likitua nchini Saudi Arabia.

“Kundi la kwanza lina Waislamu 227 wanaosafiri na kundi la mwisho la mahujaji litaondoka Juni 22,” akasema Ole Naado.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale (wa pili kushoto) akijadiliana na Mwenyekiti wa Supkem Bw Hassan Ole Naado (kulia) huku viongozi wengine wa Kiislamu pamoja na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Airways (KQ) Allan Kilavuka wakifuatilia majadiliano ya wawili hao katika uwanja wa JKIA, Nairobi mnamo Juni 16, 2023. PICHA | CECIL ODONGO
  • Tags

You can share this post!

Safaricom na Kenya Airways wamwaga mamilioni kupiga jeki...

AMINI USIAMINI: Ndege anayefahamika kama Pelegrine falcon...

T L