• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Maafisa wasaka Al-Shabaab waliojeruhi mhandisi Lamu

Maafisa wasaka Al-Shabaab waliojeruhi mhandisi Lamu

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa usalama, Kaunti ya Lamu wanaendeleza operesheni ya kuwasaka washukiwa wa kundi la Al-Shabaab waliotekeleza shambulio la kilipuzi cha kutegwa ardhini lililoacha mtu mmoja akijeruhiwa vibaya Jumamosi.

Hussein Abdi Maali, ambaye ni mhadhisi tajika, alijeruhiwa kichwani na mgongoni pale gari ambalo alikuwa ndani yake kukanyaga kilipuzi na kuharibiwa vibaya kwenye barabara ya Hindi-Bar’goni mnamo Jumamosi mchana.

Bw Abdi,50, alikuwa ametoka Bar’goni kuelekea Hindi kununua bidhaa wakati shambulio hilo lilitekelezwa majira ya saa sita adhuhuri.

Mpwa wake aliyekuwa ndani ya gari hilo, alifaulu kuruka na kutorokea msituni kabla ya kuokolewa na maafisa wa usalama.

Bw Abdi kwa sasa anapokea matibabu kwenye hospitali kuu ya King Fahd iliyoko kisiwani Lamu.

Afisa wa Utawala aliyezungumza na Taifa Jumapili na kudinda kutaja jina, alisema makabiliano makali ya risasi yalizuka kati ya magaidi na walinda usalama kabla ya magaidi hao kushi9ndwa nguvu na kutokomea msitu wa Boni.

“Magaidi walikuwa wamejipanga kuua. Baada ya kmulipua gari, walijaribu kulifikia ili kuwamaliza waliokuwa ndani. Kwa bahati nzuri, walinda usalama, wakiwemo wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya (KDF) na askari wa akiba (NPR) kutoka Bar’goni wal.ifika haraka eneo la shambulio ambapo walikabiliana vilivyo na magaidi na kuwashinda nguvu. Isingekuwa hao walinda usalama, ninaamini magaidi wangekuwa wamemuua mhandisi huyo,” akasema afisa huyo wa utawala.

Jumapili, doria za walinda usalama ziliongezwa, ambapo magari ya KDF na vitengo vingine vya usalama yalishuhudiwa yakipitapita barabarani.

Shambulio la Jumamosi lilijiri wiki mbili pekee baada ya shambulio linguine la Al-Shabaab kutekelezwa kwenye barabara hiyo hiyo ya Hindi-Bar’goni na kuacha lori likiwa limeharibiwa vibaya.

Shambulio hilo la Agosti 15 lilitekelezwa majira ya saa nne na nusu mchana, ambapo magaidi walitumia gruneti ya kurushwa kwa mbali (RPG) kuharibu lori hilo.

Aidha dereva na kpondakta wake walinusurika bila majeraha yoyote kabla ya kuokolewa na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) kutoka kituo cha polisi cha Mokowe.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, kaunti ya Lamu imeshuhudia visa vya mashambulio ya Al-Shabaab vilivyoacha watu 10 wakiuawa ilhali nyumba zaidi ya 20 zikiteketezwa na mali kuharibiwa.

Agosti 22, 2023, magaidi wa Al-Shabaab waliwachinja watu wawili, akiwemo dereva wa lori na msaidizi wake katika eneo la Lango La Simba, kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Agosti 21, 2023, magaidi wa Al-Shabaab walivamia kijiji cha Salama, Lamu Magharibi usiku, ambako walichoma nyumba nane na kanisa moja.

Kati ya Juni na Septemba 2023, vijiji, hasa vya Salama, Juhudi, Widho na viungani mwake vimekabiliwa na utovu wa usalama, hivyo kuwasukuma wakazi kutorokea kwenye kambi ya shule ya msingi ya Juhudi, iliyoko Lamu Magharibi kulala usiku na kurudi makwao mchana.

Zaidi ya familia 200 zimekuwa zikilala shuleni humo hadi sasa.

Wakati wa ziara ya kutathmini hali ya usalama kaunti ya Lamu mwezi Agosti, Waziri wa Ulinzi, Aden Duale aliapa kuhakikisha Al-Shabaab wanakabiliwa vilivyo na kutokomezwa Lamu.

Miongoni mwa mikakati ambayo Waziri Duale alitaja kwamba ingetumika kuwakabili Al-Shabaab Lamu ni kupasuliwa na kujengwa kwa njia sita za usalama msituni Boni.

Barabara hizo za usalama zitakazojengwa na KDF ni pamoja na ile ya kilomita 21 ya Witu-Pandanguo, barabara ya kilomita 40 ya Mkokoni-Kiunga, Bodhei-Kiunga, Pangani-Bodhei-Kiunga, Kiangwe-Basuba na Witu-Sendemke-Katsaka Kairu.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua: Watu kutoka Nyeri huchangamkia kazi kama fisi kwa...

Owalo azindua jopokazi la kuleta mageuzi katika sekta ya ICT

T L