• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Gachagua: Watu kutoka Nyeri huchangamkia kazi kama fisi kwa mzoga

Gachagua: Watu kutoka Nyeri huchangamkia kazi kama fisi kwa mzoga

NA MWANGI MUIRURI 

Naibu Rais Rigathi Gachagua amedai kwamba watu wa Nyeri ndio waaminifu zaidi ndani ya serikali akisema kwamba Rais mwanzilishi wa Taifa Hayati Mzee Jomo Kenyatta aliwaamini.

Alisema kwamba wakati Mzee Kenyatta alianza kuugua, ‘alikabidhi’ serikali yake kwa watu wa Nyeri na waliichunga na kuendesha kwa njia iliyomfurahisha.

“Sisi watu wa Nyeri hatutaki kujipiga kifua na hatutaki tuonekane kama tunajipendelea lakini ukweli wa mambo ni kuwa sisi ni fisi wa kazi,” akasema akiongea katika Kaunti ya Nyeri mnamo Jumamosi.

Bw Gachagua alisema hayo wakati Rais William Ruto ameonekana kuungwa mkono kwa dhati katika kusaka amani na mrengo wa Azimio na wanasiasa nje ya Kaunti ya Nyeri.

Huku Bw Gachagua akiongoza kupinga mazungumzo ya kitaifa kati ya serikali na Azimio, huku mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro pia akipinga, kinara wa wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichung’wa ameunga mkono.

Aidha, Gavana wa Embu Bi Cecily Mbarire anaunga mkono mazungumzo hayo.

Pia, mara kwa mara Rais ameonekana kumwaminia Mkuu wa Mawaziri Bw Musalia Mudavadi, akimpa majukumu nyeti kama ya kukutana na wawekezaji.

“Kujitetea huko kwa Bw Gachagua kwamba watu wa Nyeri ndio wachapa kazi na waaminifu na pia kusisitiza kwamba ana kazi ya kulinda Rais asisumbuliwe na Azimio, ni ishara tosha kwamba joto la kutengwa linazidi kupanda katika nafsi ya Gachagua,” akasema mchanganuzi wa siasa na pia mwanasiasa wa eneobunge la Kigumo Bw Zack Kinuthia.

Katika hotuba yake, Bw Gachagua alitoa mfano wa jinsi Mzee Kenyatta alivyowaamini Mwai Kibaki (Wizara ya Fedha na Mipango ya Kitaifa), Isaiah Mathenge akiwa mkuu wa mkoa wa Rift Valley na Eliud Mahihu akiwa mkuu wa mkoa wa Pwani.

Aliongeza kuwa Bw Stephen Mureithi akiwa Naibu wa Mkurugenzi wa Shirika la ujasusi nchini, Ignatius Nderi kama mkuu wa kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Matu Wamae (ICDC) na James Karundi wa Shirika la Reli nchini.

Bw Gachagua aliomba watu wa Nyeri ambao wamepewa kazi na Rais Ruto wachangamkie kazi. Aliwataka wengine watakaozidi kuteuliwa watie bidii ili kuhifadhi imani iliyoko na na nembo ya utendakazi miongoni mwao.

“Sisi tusiwe wa kuaibisha serikali. Tujitume ili tudumishe nembo yetu nzuri ndani ya serikali,” akasema

  • Tags

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Ndoa huyumba pale mume na mke wote ni...

Maafisa wasaka Al-Shabaab waliojeruhi mhandisi Lamu

T L