• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Mahakama yaokoa walipa ushuru dhidi ya kulipa wakili Sh1 bilioni Kaunti ya Kilifi

Mahakama yaokoa walipa ushuru dhidi ya kulipa wakili Sh1 bilioni Kaunti ya Kilifi

NA BRIAN OCHARO

WALIPA ushuru katika Kaunti ya Kilifi wamepata afueni baada ya Mahakama Kuu Malindi kutupilia mbeli kesi ya wakili aliyekuwa anadai malipo ya Sh1 bilioni kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo.

Jaji Stephen Githinji aliamua kuwa maombi ya wakili huyo hayakuwa na msingi na kwamba kaunti ilionyesha nia ya kujitetea katika kesi hiyo ikizingatiwa ni kiasi kikubwa cha fedha kinachohusika.

“Jambo muhimu ni kwamba hukumu ya kupeana fidia aina hii inapaswa kutolewa tu katika kesi zilizo wazi. Kwa maoni yangu, hii sio kesi kama hiyo hivyo basi ombi hilo haliwezi kukubaliwa,” alisema Jaji Githinji.

Mgogoro kati ya wakili Stephens Kithi Ngombo na kaunti, unatokana na makubaliano ambayo wakili huyo alisaidia kuandaa wakati Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi alikuwa gavana wa Kilifi.

Wakili huyo alisaidia kuandaa makubaliano kati ya kampuni ya Raindrops Ltd na kaunti mnamo 2014.

Kampuni hiyo na kaunti zimekuwa na migogoro tofauti mahakamani kuhusu ukiukaji wa makubaliano kuhusu ukusanyaji wa ushuru katika kaunti hiyo.

Kwa mfano, mwaka 2021, kaunti ilienda mahakamani kuzuia kampuni hiyo kudai zaidi ya Sh650 milioni na pia Sh2.5 milioni.

Fedha hizo zinatokana na mzozo kati ya kaunti na kampuni hiyo kuhusu uvunjaji wa mkataba wa ukusanyaji wa ushuru.

Katika kesi hiyo, kampuni hiyo iliwasilisha kesi dhidi ya kaunti, ikidai kuwa ilivunja makubaliano ya ukusanyaji wa ushuru na ada ya maegesho ambayo pande zote zilikuwa zimekubaliana.

Mnamo Septemba mwaka jana, Bw Kithi alishtaki kaunti, akitumai kupokea mabilioni ya pesa kutokana na huduma yake ya kuwezesha makubaliano kati ya kampuni hiyo na kaunti.

Bw Kithi aliiomba mahakama itoe hukumu ya haraka dhidi ya kaunti akisisitiza kuwa pesa hizo hazijalipwa kwa miaka tisa sasa.

Alihoji kwamba alitoa taarifa ya kudai malipo mnamo 2021 lakini kaunti hiyo ilidinda kufanya malipo au kutoa taarifa zozote.

“Nimeipa kaunti muda wa kutosha wa miaka tisa lakini haijafanya malipo licha ya muda wote huo,” alisema wakili.
Kupitia Martin Mwangi, kaunti ilikiri kupokea taarifa ya wakili huyo akidai malipo, lakini ikawa na wasiwasi kuhusu uhalali wa madai hayo.

Kulingana na Bw Mwangi, kaunti inapaswa kupewa nafasi ya kutetea msimamo wake mahakamani kabla ya uamuzi wowote kuhusu dai la wakili huyo kutolewa.

Bw Mwangi pia alithibitisha kwamba wakili alipokea maagizo ya kuandaa makubaliano kati ya kaunti na Rain Drops Ltd. Makubaliano haya yalifanikiwa na kusainiwa mnamo Machi 28, 2014.

“Madai yoyote ya malipo kwenye mkataba huu yalipaswa kuwasilishwa ndani ya miaka mitatu baada ya kutekelezwa kwa makubaliano hayo au tarehe ambayo kazi ya kuandaa makubaliano ilikamilika,” alisema.

Bw Mwangi pia alibaini kuwa  hakuna ushahidi katika rekodi unaoonyesha kaunti iliendelea kumshirikisha Bw Kithi katika utekelezaji wa makubaliano hayo baada ya kazi yake kukamilika.

  • Tags

You can share this post!

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa yachapisha video kuonyesha...

Naftali Kinuthia apatikana na hatia ya kumuua mwanachuo Ivy...

T L