• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa yachapisha video kuonyesha El Nino ipo nchini

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa yachapisha video kuonyesha El Nino ipo nchini

NA LABAAN SHABAAN

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya (KMD) imechapisha video mitandaoni kuelezea El Nino imeanza kushuhudiwa maeneo tofauti.

Ndani ya siku mbili zilizopita, mvua kubwa zimeshuhudiwa Kaunti ya Marsabit na kuua watu wawili katika kijiji cha Loglogo.

Hii ni baada ya Mto Malgis kuvunja kingo zake uliposhindwa kumudu nguvu za mafuriko.

Maji haya yaliwasomba watu wawili wakiwemo mzee wa miaka 90 na mtoto wa miaka mitatu waliokutana na mauti yao.

Picha zilizochapishwa na idara ya utabiri wa hali ya hewa zinaonyesha maji mengi yaliyoharibu barabara na kusababisha mmomonyoko wa udongo.

Kwa hivyo, shughuli za kawaida za maisha ikiwemo usafiri umetatizwa huku miti, makazi ya watu na mifugo ikisombwa.

Kituo cha KMD Marsabit kilinakili mvua kiwango cha 55.6mm Jumanne Oktoba 24, 2023 na Jumatano Oktoba 25, 2023.

Katika taarifa ya tukio jingine, ajuza mmoja wa miaka 70 alifariki Kaunti ya Busia katika eneobunge la Teso Kaskazini.

Wakazi wanasema mvua ya kiwango cha kadri iliandamana na upepo mkali ulioangusha miti na kuharibu nyumba.

Hali hii imesababisha zaidi ya familia 50 kukosa makazi.

Kwingineko, matawi kadhaa ya KMD Kaunti ya Meru, yamerekodi mvua kubwa za 25.4mm zilizosababisha mafuriko na masumbuko.

Mnamo Oktoba 24, 2023 idara ya utabiri wa hali ya hewa ilithibitisha kuwa mvua kubwa ziliponda maeneo ya Igembe ya Kati hasaa Shule ya Msingi ya Nguthukii.

Mvua hizi zimevuruga shughuli za kawaida katika kijiji cha  Kirindine, Wadi ya Kianjia iliyoko Tigania Magharibi, Igembe Kaskazini.

Masomo katika Shule ya Upili ya Lower Chure Imenti Kusini yalitatizika sababu ya mafuriko.

Pia, KMD imenakili mvua kiwango cha 11.5mm eneobunge la Imenti Kusini.

Ripoti za kujiri kwa mvua hizi zinajiri baada ya serikali kutangaza hakutakuwa na El Nino kama ilivyotabiriwa awali.

Mnamo Oktoba 22, 2023, Jumapili iliyopita, Rais William Ruto alisema kwamba idara ya hali ya anga ilitoa habari kuwa badala ya El Niño, kutakuwa na mvua kubwa.

“Hata juzi mliskia huenda kukawa na El Nino ambayo itaharibu mali. Lakini Mungu ni nani! Mmesikia wale watu (Idara ya Hali ya Hewa) wamesema hiyo El Nino haitakuwepo. Wamesema kutakuwa tu na mvua kubwa, lakini haitafika pale pa kuharibu. Si tunamshukuru Mungu jamani?” Rais alisema.

Kaunti zilitenga angalau Sh15 bilioni kukabili na kudhibiti athari za mvua hizo huku zaidi ya Sh10 bilioni zikiratibiwa kutumiwa kudhibiti hali katika maeneo kame.

Lakini, inaripotiwa kuwa baada rais kutangaza kutokuwepo kwa mvua za El –Nino, hazina hizi zilihamishwa kwa shughuli nyingine za serikali.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya waelezea kumkosa Rais Mstaafu Kenyatta huku...

Mahakama yaokoa walipa ushuru dhidi ya kulipa wakili Sh1...

T L