• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Naftali Kinuthia apatikana na hatia ya kumuua mwanachuo Ivy Wangeci miaka minne iliyopita

Naftali Kinuthia apatikana na hatia ya kumuua mwanachuo Ivy Wangeci miaka minne iliyopita

NA TITUS OMINDE

Mahakama Kuu mjini Eldoret mnamo Alhamisi Oktoba 25, 2023 ilimpata Naftali Kinuthia, 33, na hatia ya kumuua mpenzi wake ambaye alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Moi, Ivy Wangeci miaka minne iliyopita.

Bw Kinuthia ambaye ni mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano alipatikana na hatia na Jaji Reuben Githinji.

Kupitia kikao cha mtandaoni kati ya mahakama kuu ya Malindi ambapo Jaji Githinji amehamishwa na Gereza kuu la Eldoret, Jaji Githinji aliamua kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka ya mauaji dhidi ya mshtakiwa.

Bw Kinuthia alisimulia mahakamani jinsi alivyokuwa akimsaidia mpenzi wake aliyeuawa kwa ajili ya kumtunza alipokuwa katika chuo kikuu ikiwa ni pamoja na kufadhili karamu zake za kuzaliwa.

Siku ya maafa mnamo Aprili 2019, alisema kwamba alisafiri kutoka Thika ambako alikuwa akifanya kazi hadi Eldoret kwa kile ambacho kingekuwa ziara ya ghafla kwa mpenzi wake wa muda mrefu siku yake ya kuzaliwa.

Katika hali ya kushangaza, mambo yaligeuka kuwa mabaya kati ya wawili hao baada ya mwathiriwa kudaiwa kukataa penzi lake, na kumfanya amkate na shoka hadi kufa.

“Siku ya maafa asubuhi, niliondoka kwa mita chache na kugeuka nyuma, nilimwona mpenzi wangu akikumbatiana na mwanaume mwingine, ‘Siwezi kusema hata wakati niliamua kuokota shoka kwenye gari langu ambalo nilikuwa nimepaki karibu. Sikuwa mimi mwenyewe,” akasimulia Bw Kinuthia.

Alikuwa amemweleza jaji kuwa alijuta juu ya tukio hilo huku akimshutumu mpenzi wake wa siku nyingi kwa kumtumia visivyo kujinufaisha kifedha.

“Ninajutia kifo cha Ivy kwani hakuwa na hatia. Kuna njia nyingi ambazo tungeweza kutatua tofauti zetu badala ya kumuua,” akasema Bw Kinuthia.

Upande wa mashtaka ulifunga kesi yake Juni 2022 huku Serikali ikiwasilisha mashahidi zaidi ya 10 miongoni mwao mama na wajomba wawili.

Bw Kinuthia atajitetea Novemba 22 kabla ya kuhukumiwa.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yaokoa walipa ushuru dhidi ya kulipa wakili Sh1...

Tineja akiri kuua afisa mkuu wa fedha wa Nairobi Hospital,...

T L