• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Makala ya msanii wa nyimbo za injili Mary Njuguna

Makala ya msanii wa nyimbo za injili Mary Njuguna

NA PATRICK KILAVUKA

Mapito na changamoto za maisha zilimchochea kuwahimiza wengine, kuwainua kiimani na kumtumainia Mola zaidi kupitia nyimbo zake za injili.

Isitoshe, talanta yake imempanua kuelewa mambo kwa njia ya kiasilia na kiroho. Mbali na injili kuwa inaokoa, inakomboa na kutoa suluhisho ya matatizo pamoja na kusawazisha mambo.
Hiyo ni kauli ya mwimbaji wa nyimbo za injili Mary Njuguna 25.

Alizaliwa eneo la Ndeffo, kaunti ndogo ya Njoro, Kaunti ya Nakuru. Yeye ni mtoto wa watano katika familia ya watoto sita wa Bw James Njuguna  na Bi Anne Mukami.Alipata uwezo wa kusoma hadi darasa la nane, Shule ya Msingi ya Ndeffo na kwa sababu ambazo hangeziepuka za kikaro, hakuendelea kielimu ila, aliguria Nairobi kwa mujibu wa kusaka kibarua na akafua dafu kuwa mjakazi.

Japo aliambulia kupata mchumba na kuolewa, anadokeza kwamba changamoto za kindoa zilimpa mbinu mbadala za kusawazisha maisha kwani, alikuja kuona kwamba pasi na Maulana ambaye amemtegemea dira ya maisha ingeweza kupotea.

Hivyo basi, kwa kuamua kushikilia uzi wa wokovu na kudumisha talanta yake ya uimbaji, amejizatiti kupitia nyimbo zake kutoa ujumbe wa tumaini kwa asasi za kijamii.Suala la uimbaji alilianza akiwa shule ya chekechea kwao Ndeffo ambako alikuwa pia mfuasi wa kanisa la AlPECA.

Msanii wa nyimbo za injili Mary Njuguna akiimba…PICHA/PATRICK KILAVUKA

Alikuwa kiongozi wa nyimbo katika ibada za watoto.Baada ya kumaliza masomo ya msingi, mwimbaji huyu anasema alipitia mapito ya kuvujwa moyo,  kukatalia na kupoteza matumaini maishani.

Lakini alijipa moyo kulisoma Neno la Mungu ambalo lilimpa ushauri mkubwa wa mbinu na silaha za kukabiliana na pandashuka za maisha. Mbali na kulizamia, amelitumia kujenga wengine na kuwatia moyo kwa kutambua kuwa Maulana ni wa fursa nyingine katika maisha na kuteleza si kuanguka!

Mwaka wa 2014, alianza kutunga nyimbo ambazo zimemfungulia milango ya neema ya uimbaji.
Amezirekodi nyimbo sita ambazo zinapatikana kwenye mtandao wa Youtube Marynjuguna.
Tungo zake ni Wigocithia (Jitukuze nami), Turiruaga na Mirii ( Hatupigani vita vya mwili), Amukira Gatho ( Pokea sifa),Twarana nanii ( Pelekana nami) Ningwendete ( Nakupenda Yesu) na Ni wega Ngai (Asante Mungu).

Nyimbo tatu za kwanza zina video.Kwa vile azma yake ni kuendeleza injili, nyimbo huziangazia kwenye majukwaa ya sherehe, makanisani na makrusedi japo ujio wa ndwele ya corona, ulileta kizungumti kidogo.

Anasema haimbi tu nyimbo zake bali zimekuwa za baraka hata kwake mwenyewe kwa sababu zimemkuza kiroho na kiimani. Isitoshe, zimempelekea kusonga karibu na Mwenyezi Mungu na kumpa tumaini la hatua kwa hatua maishani.

Mwimbaji ambaye hupenda nyimbo zake ni Shiro wa GP.Angependa kumshukuru msanii/ produsa Steve Macharia kwa kusimama naye kiusanii na ushauri jinsi anavyoweza kujikuza kiusanii.Angependa sana kutangaza injili kimataifa kwa minajili ya kufikia wengi.

Ushauri wake ni kwamba waimbaji wawe waaminifu kwa Muumba wakimtumainia katika kila hali na wakumbuke kwamba, japo wanaweza kuteleza wasikae mavumbuni mbali wayakungute na wapeleke injili mbele!

  • Tags

You can share this post!

Umoja na KPA zashinda kwenye pambano la primia

Jifunze kuandaa pankeki tamu za matunda ya blueberries