• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:46 PM
Mamilioni ya fedha Kenya imetumia katika Safari Rally ikitafuta kuvuna mabilioni, kujenga jina

Mamilioni ya fedha Kenya imetumia katika Safari Rally ikitafuta kuvuna mabilioni, kujenga jina

Na GEOFFREY ANENE

KENYA inatarajia kuvuna Sh6 bilioni mbali na fahari na kujinadi kimataifa kutokana na kuandaa duru ya Safari Rally inayorejea kwenye ratiba ya Mbio za Magari Duniani (WRC) baada ya miaka 19 hapo Juni 24-27.

Hata hivyo, gharama ya kuwa mwenyeji wa duru ya WRC ya Safari Rally si fedha chache.Ripoti mbalimbali zinasema serikali imewekeza zaidi ya Sh216 milioni katika makala haya ya 68 ya Safari Rally ambayo madereva 58 watashiriki.

Kampuni za kibinafsi kama shirika la ndege la Kenya Airways, kampuni ya magari ya Toyota Kenya, benki ya KCB, kampuni ya mawasiliano ya Safaricom na kampuni ya kamari ya Betika mamilioni ya fedha kusaidia Safari Rally moja kwa moja ama kusaidia madereva.

Mnamo Mei 6, Afisa Mkuu wa WRC Safari Rally Phineas Kimathi alieleza wanahabari kuwa Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA) limeitisha helikopta 15 kutumika wakati duru hiyo ya sita kati ya 12. Helikopta moja inauzwa kwa kati ya Sh200 milioni na Sh340 milioni kutegemea na upya wake.

Kwa mujibu wa afisa mmoja kutoka uwanja wa ndege wa Wilson hapa jijini Nairobi, kukodisha helikopta moja ni Sh200,000 kwa saa moja. Hii inamaanisha kuwa wenyeji watalipia Sh19.2 milioni wakiamua kukodisha helikopta hizo 15 kwa siku hizo nne za mashindano.

Aidha, waandalizi wa Safari Rally wamesema wanatarajia watu 850 milioni kutoka mataifa 150 kutazama mbio hizo kupitia runinga.Safari Rally inarejea kwenye WRC baada ya miaka 19. Kenya ilipoteza hadhi yake ya WRC mwaka 2003 kutokana na ukosefu wa fedha kabla ya kufanya kampeni kali mwaka 2018 ikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kufaulu kuipata tena 2020 baada ya kuridhisha katika majaribio 2019.

Takwimu nyingine muhimu katika mashindano haya ni kuwa zaidi ya maafisa 1,000 wa usalama wataweka doria.Idadi hiyo pia inajumuisha waelekezi (marshals) wa barabarani wameajiriwa kuhakikisha mashindano haya ni salama.

Zaidi ya watu 2,500 wanaohusika moja kwa moja na Safari Rally wakiwemo maafisa kutoka serikalini, wanatarajiwa kuhudhuria mashindano haya. Ukubwa na umuhimu wa mashindano haya umeshuhudia hoteli zote za kisasa 60 katika eneo la Naivasha zikikodishwa na wageni.

Vilevile, kurejea kwa Safari Rally kumeshuhudia serikali ikianzisha kampeni ya kupunguza joto duniani kupitia upanzi wa miti. Inapanga kupanda jumla ya miti 19 milioni katika maeneo ya zamani yaliyotumia kwa Safari Rally. Maeneo hayo ni Kilifi, Mombasa, Kwale, Taita Taveta, Machakos, Makueni, Murang’a, Meru, Nyeri, Embu, Kirinyaga, Kiambu, Kajiado, Laikipia, Isiolo, Narok, Nakuru na Nairobi pamoja na msitu wa Kakamega na eneo la Ziwa Victoria.

Madereva watawania alama za WRC, huku Wakenya pia wakitafuta zile za kitaifa katika mbio hizo zinazojumuisha kilomita 320.19.Mashindano yenyewe yanayotarajiwa kuanzishwa na Rais Kenyatta nje ya Jumba la KICC, yatafanyika katika maeneo ya Kasarani, Chui Lodge, Kedong, Oserian, Elementaita, Soysambu, Sleeping Warrior, Loldia, Hell’s Gate na Malewa.

Madereva wote 58 wanaotarajiwa kushindana akiwemo raia wa Estonia, Ott Tanak, wamekuwa na shughuli nyingi Juni 21 na Juni 22 kujifahamisha na barabara za mashindano katika maeneo ya Naivasha. Bingwa wa dunia Sebastien Ogier, ambaye pia anaongoza mashindano ya 2021, yuko katika orodha ya madereva wanaopigiwa upatu kushinda Safari Rally.

Madereva wanaoshiriki duru zote za WRC wanaaminika kuwa na magari yanayogharimu Sh120 milioni.Chipukizi McRae Kimathi, Hamza Anwar na Jeremy Wahome wataendesha magari mapya kabisa ya Ford Fiesta yanayogharimu Sh13 milioni kila moja.

Duru nyingine zitakazofuata Safari Rally ni Estonia (Julai), Ubelgiji (Agosti), Ugiriki (Septemba), Finland (Oktoba), Uhispania (Oktoba) na Japan (Novemba). Madereva wa WRC wameshakamilisha duru tano ambazo ni Monaco (Januari), Finland (Februari), Croatia (Aprili), Ureno (Mei) na Italia (mapema Juni).

 

  • Tags

You can share this post!

Wakenya 36 kuwakilisha taifa Riadha za Dunia za Viziwi...

Ana maono ya kucheza soka ya kulipwa