• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Man-U wanaweza kumaliza nne-bora EPL?

Man-U wanaweza kumaliza nne-bora EPL?

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United waliendeleza rekodi nzuri ya kutopigwa katika mechi 24 ugani Old Trafford msimu huu baada ya kutandika Everton 2-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mabingwa hao mara 20 wa EPL walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Scott McTominay katika dakika ya 36 kabla ya Anthony Martial kuwafungia la pili baada ya kushirikiana vilivyo na Marcus Rashford kunako dakika ya 71. Bao la Martial lilikuwa lake la kwanza ligini tangu Disemba 2022.

Everton walijitosa ulingoni baada ya kutoshana nguvu na Tottenham Hotspur kwa sare ya 1-1 katika mechi yao ya awali na kuweka hai matumaini finyu ya kukwepa shoka la kuwateremsha ngazi kutoka EPL hadi Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) msimu ujao.

Man-United kwa upande wao walishuka dimbani wakiwa na ulazima wa kushinda kadri wanavyolenga kukamilisha kipute cha EPL muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora. Sasa wanajivunia alama 56 baada ya kushinda mechi 17, kupiga sare tano na kupoteza michuano saba kati ya 29 ligini muhula huu.

Ushindi dhidi ya Everton unatarajiwa sasa kutambisha Man-United wanaofukuzia mataji mawili zaidi msimu huu baada ya kucharaza Newcastle United 2-0 na kujizolea ubingwa wa Carabao Cup mwishoni mwa Februari ugani Wembley.

Masogora hao wa kocha Erik ten Hag wataalika Sevilla kwa mkondo wa kwanza wa robo-fainali za Europa League mnamo Alhamisi ugani Old Trafford kabla ya kuendea Nottingham Forest ligini kisha kutua Uhispania kwa mkondo wa pili wa Europa League.

Baada ya hapo, Ten Hag ataongoza waajiri wake kupepetana na Brighton kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA uwanjani Amex kabla ya kufunga kampeni ya Aprili ligini kwa kibarua kizito dhidi ya Spurs na Aston Villa mtawalia.

Kwa kutandika Everton jana, Man-United sasa hawajapoteza mechi 24 mfululizo katika uga wao wa nyumbani tangu Septemba 2022 ambapo Real Sociedad ya Uhispania iliwakomoa 1-0 katika mojawapo ya mechi za Kundi E kwenye Europa League.

Mechi 13 kati ya hizo ambazo zimeshuhudia Man-United wakikwepa kichapo nyumbani zimekuwa za EPL. Kikosi hicho pia hakijafungwa bao katika mechi nne zilizopita ugani Old Trafford.

Everton kwa upande wao walijibwaga ulingoni wakipigiwa upatu wa kujinyanyua dhidi ya Man-United baada ya kocha Sean Dyche kuwaongoza kushinda mechi moja na kupiga sare tatu dhidi ya Nottingham Forest, Brentford, Chelsea na Spurs.

Alama 27 ambazo wameokota kutokana na mechi 30 zinawaacha wakikodolea macho hatari ya kushushwa ngazi ikizingatiwa kwamba wametandaza michuano miwili zaidi kuliko Leeds United na Crystal Palace watakaomenyana leo uwanjani Elland Road. Palace wanajivunia alama 30, moja kuliko Leeds.

Everton sasa hawajashinda mechi yoyote kati ya 11 zilizopita katika EPL ugenini na wamefungwa angalau mabao mawili katika kila mojawapo ya mechi sita za sampuli hiyo ligini.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa msimu huu kupulizwa, Everton walikuwa wamekwepa kichapo kutoka kwa Man-United mara tatu mfululizo. Hata hivyo, sasa wamepigwa na miamba hao mara tatu muhula huu. Hadi kufikia juzi, walikuwa wametandikwa 2-1 katika EPL na 3-1 katika raundi ya tatu ya Kombe la FA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

AFYA NI MTAJI: Dalili hizi huenda zikaashiria una kansa ya...

Ulevi, magonjwa ya akili yatatiza walimu shuleni –...

T L