• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Kuku wageuka dhahabu Desemba 2023

Kuku wageuka dhahabu Desemba 2023

NA SAMMY WAWERU

KILA Desemba, ulimwengu huungana kuadhimisha siku maalum ya kuzaliwa kwa Yesu Kristu inayofanyika tarehe 25.

Mwezi wa Desemba ukianza, shamrashamra za sherehe nazo zimeanza kubisha hodi.

Kila boma Kenya na ulimwengu kwa jumla, familia nyingi hukongamana kusherehekea.

Desemba 25, 26 na makaribisho ya mwaka mpya, Januari 1, milo ya kipekee huandaliwa.

Huku msimu huo ukikaribia, bei ya mifugo hasa inayolengwa sana kwa minajili ya kitoweo cha nyama imeanza kupanda.

Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali umebainisha kuwa bei ya kuku haikamatiki.

Hata ingawa mfumuko wa bei ya chakula cha madukani cha mifugo unachangia, wafugaji na wafanyabiashara wa kuku hasa wanaochinja wanapandisha bei ili kuvuna faida.

Nyongeza hiyo inatokana na mahitaji ya kuku msimu wa Krismasi.

Kuku kwenye kizimba cha mfanyabiasha Zimmerman, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Susan Njoroge, mfanyabiashara katika mtaa wa Zimmern, Nairobi anasema mwaka huu, 2023, uuzaji kuku umenoga.

Aidha, amekuwa katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka mitano.

Kuku mwenye uzani wa kilo mbili hapungui Sh800, juu kutoka Sh600 na Sh700 bei ya hapo awali.

Anafasiri Krismasi inapokaribia, huenda bei ikakwea hadi Sh1, 000.

Susan anadokeza kwamba hutoa kuku wake kutoka kwa wafugaji na wauzaji wa kijumla.

Wale wa kienyeji walioboreshwa, bei inaendelea kupanda Antony Mwangi, muuzaji kuku eneo la Ruiru, Kiambu, akisema, “Kuku halisi wa kienyeji bei ya chini tunayouza ni Sh1, 000 kwa sasa na huenda ikapanda hadi Sh1, 500 – mwenye uzani wa kilo 1.5.”

Bei ya kuku imeanza kuongezeka msimu huu wa Krismasi 2023. PICHA|SAMMY WAWERU

Mabadiliko hayo ya bei yanashuhudiwa katika mitaa mingi Nairobi na Kiambu, inayojumuisha Zimmerman, Ruiru, Githurai, Kahawa West, Mwiki, Thika, Wangige, Uthiru, kati ya mingine.

Kevin Kilonzo, mfugaji Juja, Kaunti ya Kiambu, anasema mfumuko huo wa bei si jambo geni.

Kulingana na Kilonzo, Desemba wanunuzi huwa hawalalamiki, jukwaa ambalo wakulima hutumia kurejesha mapato yaliyowachenga.

Isemavyo, kufurahia na kujiburudisha huja na gharama.

Ikiwa unapanga kujiburudisha wewe na familia yako kwa nyama ya kuku, msimu huu wa Krismasi, ni vyema kuweka kando bajeti kwa ajili ya shughuli hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Watumiaji TikTok kuanza kuchuma hela na zawadi

Masoja walalamikia kufungiwa chooni na wahalifu wizi...

T L