• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mawakili waliotapeli mwekezaji wa kigeni mamilioni wakabiliwa

Mawakili waliotapeli mwekezaji wa kigeni mamilioni wakabiliwa

NA RICHARD MUNGUTI

MZOZO mpya unatokota kati ya mwekezaji kutoka Rwanda Desire Muhinyunza na mawakili waliomwakilisha aliyekuwa mfanyabiashara mwenza, Kirimi Koome kuhusu kashfa ya Sh74.3 milioni.

Bw Muhinyunza amefichua kwamba Oktoba 30, 2023 mawakili Omwanza Nyamweya na Ivy Ateko Ingati walipata agizo la mahakama kwa njia ya ufisadi wakikubaliwa kuweka katika akaunti zao Sh74, 300, 000.

Mwekezaji huyo amelalamika kuwa mawakili hao wawili walipotosha mahakama na kwamba wamefanya uhalifu kuweka pesa za wateja wanaofanya biashara katika mtandao wa Stay Online Limited (SOL).

Mawakili hao walikuwa wanamtetea Bw Koome katika kesi ya ufisadi inayomkabili na pia katika Mahakama Kuu.

Kupitia kwa Wakili Danstan Omari, Bw Muhinyunza ameomba Idara ya Upelelezi wa Uhalifu na Jinai (DCI) iwachunguze mawakili hao wawili; Omwanza na Ateko kwa kupotosha mahakama kupata agizo wakate pesa za wateja kuwa ada yao ya kumtetea Bw Koome.

Katika barua kwa DCI na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Omari ameomba uchunguzi ufanywe kwa lengo la kuzuia wizi wa Sh74, 300, 000.

“Omwanza na Ingati walificha ukweli kuhusu umiliki wa kampuni ya SOL ndipo wakapata agizo la kukata fedha Sh74.3 milioni kama ada yao ya kumtetea Bw Koome,” Bw Omari amesema.

Wakili huyo amewaeleza DCI na DPP kwamba Jaji Alfred Mabeya amemtangaza Bw Muhinyunza kuwa mmiliki wa SOL na wala sio Bw Koome.

Jaji Mabeya alisema katika uamuzi aliotoa Desemba 27, 2023 kwamba Bw Koome alifanya ufisadi alipoandikisha SOL kwa kutojaza fomu ya wahisani wa kampuni hiyo.

“Bw Koome alificha habari muhimu kuhusu wakurugenzi na wahisani wa SOL alipoisajili Aprili 14, 2023. Huu ni ufisadi na kamwe hastahili kumiliki kampuni hii,” Jaji Mabeya alisema.

Baada ya kutimuliwa kwenye kampuni hii na Mahakama Kuu, Bw Koome aliamriwa arudishe Dola za Amerika ($) 100, 000 (sawa na Sh15.6 milioni) alizokuwa amejipatia kutoka kwa Muhinyunza akidai ni ada ya kodi.

Pia serikali iliamriwa Desemba 29, 2023 imrudishie Muhinyunza Dola ($)2.6 milioni (Sh400 milioni) ilizokuwa imetwaa sizitumiwe vibaya na Bw Koome.

Na wakati huo huo Jaji Josphine Wayua Mong’are aliamuru kesi kuhusu pesa hizo Sh74.3 milioni itajwe mbele ya Jaji Mabeya Januari 3, 2024.

Katika kesi hiyo, Bw Muhinyunza anaomba mawakili hao washurutishwe kurudisha pesa hizo.

Pia Bw Muhinyunza anaomba mawakili hao wachunguzwe kwa lengo la kushtakiwa kwa uhalifu.

  • Tags

You can share this post!

Utafungwa jela miezi mitatu kwenda haja hadharani

Mayatima wa Jubilee wanavyojifufua kisiasa

T L