• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Mayatima wa Jubilee wanavyojifufua kisiasa

Mayatima wa Jubilee wanavyojifufua kisiasa

NA CHARLES WASONGA

TANGAZO la wabunge wa zamani wa Jubilee kwamba wataongoza msururu wa mikutano ya uhamasisho katika eneo hilo 2024 limefasiriwa kama sehemu ya mikakati yao ya kujifufua kisiasa.

Juzi, wandani hao wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, waliopoteza viti vyao katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 walikutana na viongozi 500 wa mashinani katika Kaunti ya Kiambu “kujadili sera za serikali zinazowaumiza raia.”
Duru zilisema kuwa masuala makuu yaliyojadiliwa katika mkutano huo uliofanyika katika Shule ya Upili ya Kiambu, na kuongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Limuru Peter Mwathi, ni gharama ya maisha na hatua ya serikali ya kutelekeza miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Bw Kenyatta.
“Ndio tulikutana na viongozi wa mashinani, na tutaendeleza mikutano hiyo mwaka ujao, 2024. Lakini dhima kuu ya mkutano wetu ilikuwa ni kutoa uhamasisho kwa raia kuhusu athari za sera mbovu za serikali. Ni wazi kupandishwa kwa ushuru ndiko kumechangia kupanda kwa gharama ya maisha. Pia tulifahamisha kuwa baadhi ya changamoto zinazowasibu zinatokana na kukwamishwa kwa miradi kadha ya barabara na ujenzi wa bwawa la Karemenu lililoko Gatundu Kaskazini,” anasema Bw Mwathi, ambaye alihudumu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama katika bunge lililopita la 12.
Wakati wa mkutano huo, wabunge hao wa zamani, na madiwani, walioshindwa na wagombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), walikariri kwamba wangali wanamtambua Bw Kenyatta kama msemaji wa siasa wa Mlima Kenya.
Ndiposa aliyekuwa mbunge wa Kiambu Jude Jomo akatumia jukwaa hilo kuwaonya wanasiasa wa UDA dhidi ya kile alichodai ni mienendo yao ya kumkosea heshima kiongozi huyo wa Jubilee.

“Tuliweka wazi, na viongozi wa mashinani wakakubaliana nasi kwamba, Uhuru angali kiongozi wetu na tutafanya kila tuwezalo kumkinga dhidi ya limbukeni wa kisiasa wenye tabia mbaya ya kumrushia maneno ya kumdunisha,” anaeleza.
Wachanganuzi wa siasa za Mlima Kenya wanasema kuwa wanasiasa hao wanatumia suala la kupanda kwa gharama ya maisha na jina la Bw Kenyatta kujifufua kisiasa.
“Mwaka mmoja baada ya wao kushindwa katika uchaguzi mkuu uliopita, wabunge hawa wa zamani wameng’amua kuwa wasipopaaza sauti zao, watasahaulika katika ulingo wa siasa. Hii ndio maana wamejitokeza na mada kama kupanda kwa gharama ya maisha, kutokamilishwa kwa miradi iliyoanzishwa na Uhuru Kenyatta kujaribu kujinadi kama watetezi wa raia,” akasema Gitile Naituli.
“Aidha, wamejitokeza kama watetezi sugu wa Uhuru kutokana na lawama ambazo amekuwa akielekezewa na wakuu wa Kenya Kwanza; kuanzia Rais Ruto mwenyewe,” anaongeza mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Multi Media.
Lakini kwa upande wake Herman Manyora anasema kuwa ni haki ya wanasiasa hao kujitokeza na kuzungumzia masuala yanayoathiri raia.
“Suala kama vile, kupanda kwa gharama ya maisha linaathiri Wakenya wote na ni wajibu wa viongozi hao kulizungumzia. Kushindwa kwao katika uchaguzi mkuu wa 2022 hakumaanishi kuwa sasa wanafaa kufyata hadi 2017 uchaguzi mwingine utakapoandaliwa,” anaeleza.
Lakini, kulingana na Bw Manyora, wakati kama huu ambapo raia wengi wameanza kupoteza imani kwa utawala wa Kenya Kwanza, ndio faafu kwa wanasiasa wa Mlima Kenya waliopoteza katika uchaguzi uliopita kujifufua.
“Hali ni kinyume na walivyoahidiwa nyakati za kampeni. Gharama ya maisha imepanda huku wafanyabiashara na wale wenye ajira wakizongwa na mzigo wa ushuru. Hii ndio maana juzi Uhuru mwenyewe alisema kuwa watu wengi wanampigia simu wakilalamikia ugumu wa maisha,” anaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Mawakili waliotapeli mwekezaji wa kigeni mamilioni...

Kalonzo Musyoka amesota

T L