• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Mganga aliyemtapeli Mungatana Sh76m kujitetea Jumanne ijayo

Mganga aliyemtapeli Mungatana Sh76m kujitetea Jumanne ijayo

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Chad ambaye mahakama ya Milimani Nairobi imesema yuko na kesi ya kujibu kwa kumlaghai Seneta wa Tana River Danson Mungatana(pichani) Sh76 milioni akitumia nguvu za ndumba ataanza kujitetea Septemba 26,2023.

Hakimu mkazi Ben Mark Ekhubi aliahirisha zoezi la Abdoulaye Tamba Kouro kuanza kujitetea jana kwa vile kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki hakuwa kazini.

Bi Kariuki anahudhuria warsha ya siku mbili na hivyo basi kesi hiyo haingeongozwa na kiongozi mwingine wa mashtaka kwa vile ndiye ameiendeleza tangu Kouro ashtakiwe.

Hakimu aliombwa aahirishe kesi hiyo hadi Septemba 26, 2023 , Bi Kariuki atakapokuwa kazini.

Bw Ekhubi alimweka Kouro kizimbani kujitetea baada ya upande wa mashtaka kukamilisha zoezi la kuwaita mashahidi.

Bw Ekhubi alisema upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha korti kumweka Kouro kizimbani kujitetea.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote hii mahakama imefikia uamuzi kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuwezesha mshtakiwa kuwekwa kizimbani kujitetea,” alisema Bw Ekhubi.

Alipotoa ushahidi kortini Mungatana alieleza hakimu alianza kumpa mshtakiwa idadi ndogo ya pesa alizozifanya kuongezeka maradufu ndipo akaamini anaweza kuzifanyia biashara na kuzalisha faida.

Alianza kwa kumpa Sh1 milioni zikafanywa Sh2 milioni.

Seneta huyo alieleza mahakama kuwa alimpa tena Sh5 milioni zikafanyiwa zikawa Sh10 milioni.

Lakini Mungatana alipompa Kouro Sh76 milioni alifunga simu na kutoweka.

Seneta huyo alisema mshtakiwa alisakwa kwa udi na ufumba hadi pale alipokamatwa na maafisa wa polisi wa kikosi kilichovunjwa cha Flying Squad.

Kouro anakabiliwa na mashtaka ya kumlaghai Muungatana Sh76 milioni kati ya Aprili 20, 2011 na Aprili 29, 2013 katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.

Mungatana aliambia mahakama aliamua kujitokeza hadharani kwa vile karibu ulaghai umsukume katika hali ya uchochole.

Pia Kouro alishtakiwa kupatikana na pesa feki za kigeni sawa na Sh960,120,000.




  • Tags

You can share this post!

Mshukiwa wa mauaji ya kikatili ya Afisa Mkuu wa Fedha...

Waumini wabaki na mshtuko kanisa la thamani ya Sh650...

T L