• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Waumini wabaki na mshtuko kanisa la thamani ya Sh650 milioni likiamuriwa libomolewe

Waumini wabaki na mshtuko kanisa la thamani ya Sh650 milioni likiamuriwa libomolewe

Na STANLEY NGOTHO

HUENDA Kanisa la PCEA Kitengela kaunti ya Kajiado lenye thamani ya Sh650 milioni likabomolewa baada ya Mahakama Kuu kuamua kwamba, limejengwa katika ardhi inayomilikiwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa za kuuza ng’ambo almaarufu EPZ.

Katika uamuzi uliosababisha mtafaruku na hofu kuu miongoni mwa washiriki zaidi ya 2,000, Jaji Maxwell Gicheru alisema kanisa hilo limejengwa katika ardhi inayomilikiwa na EPZ.

Na wakati huo huo, Jaji Gicheru aliipa Kanisa hilo muda wa siku 60 (miezi miwili) kuondoka katika ardhi hiyo baada ya kushindwa katika kesi iliyochukua muda wa miaka tisa kusikizwa.

Lakini wasimamizi wa kanisa hilo waliwapa matumaini washiriki kwa kusema watakata rufaa kupinga uamuzi huo waliosema umetishia kuipokonya ardhi iliyostawishwa kwa zaidi ya Sh6.5 bilioni.

Katika uamuzi huo uliotolewa Alhamisi, Jaji Gicheru, wa kitengo cha Mahakama Kuu cha kutatua mizozo ya Ardhi kaunti ya Kajiado alikubaliana na EPZ kwamba, kanisa hilo limejengwa katika ardhi isiyo yake.

Kanisa hilo la PCEA lilishtaki EPZ katika Mahakama Kuu, baada ya wasimamizi wa shirika hilo la serikali la kutengeneza bidhaa za kuuza ng’ambo kudai ardhi hiyo. Katika ardhi hiyo ya hektari moja, pia kuna shule yenye sifa kuu kutokana na matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa. Shule hiyo ina wanafunzi 936.

Mnamo Alhamisi, washirika walikusanyika katika ukumbi wa Kanisa hilo la PCEA kusikiza uamuzi uliosomwa kwa njia ya mitandao na Jaji Gicheru.

Washiriki walifuata uamuzi huo uliopeperushwa katika Televisheni kubwa mle ukumbini. Waumini, wakiongozwa na Kasisi Hezekiah Murage, walitulia tuli na kunyamaza Jaji Gicheru alipotamka: “Kanisa hili limejengwa katika ardhi ya EPZ.”

Kwa muda, kimya kingi kilitanda huku Kasisi Murage na waumini wakitafakari uamuzi huo uliowapiga kama radi na kutishia kuyumbisha imani yao.

Nyuso za waumini zilijaa huzuni na kukumbwa na mtafaruku walipotazama kanisa lao huku wakiwaza na kuwazua kwamba litabomolewa.
Kanisa hilo limejengwa kwa ustadi mkuu na kurembeshwa kwa mawe ya thamani kuu. Kwa mukhutasari, Jaji Gicheru alisema: “Mshtakiwa (EPZ) amethibitisha Serikali iliipea ardhi hiyo ya hektari moja mnamo Septemba 13,1991 na kwamba, hakuna mahakama au jopo la kisheria lililofutilia mbali umiliki huo,” alisema Jaji Gicheru. Jaji huyo alisema mmiliki wa zamani wa ardhi hiyo alifidiwa ipasavyo kisha akahama.

“Imethibitishwa kwamba, Serikali ilipata kwa njia halali ardhi hii mnamo 1991. Hakuna namna ardhi hii ingelisajiliwa kwa mtu au shirika lingine,” Jaji Gicheru alisema katika uamuzi huo.

Jaji huyo alisema EPZ imethibitisha kwamba, kuna tangi lake la maji lililojengwa 1991-1994 ardhi hiyo ilipouzwa.

Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, kanisa hilo lilijengwa kwenye ardhi hiyo mnamo 2002.

Licha ya afisi ya usajili wa mashamba kuwasilisha ushahidi kwamba hati miliki ya shamba hilo limesajiliwa kwa jina la PCEA, Jaji Gicheru alisema hatimiliki hiyo ilichukuliwa kwa njia ya ufisadi.

Miaka ya awali, PCEA lilikuwa limeuzia watu binafsi sehemu ya ardhi na wamestawisha sehemu zao.

  • Tags

You can share this post!

Mganga aliyemtapeli Mungatana Sh76m kujitetea Jumanne ijayo

Mwanamume mpenzi wangu alichovya nje nikamtema, sasa nahisi...

T L