• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Mganga wa Chad aliyeambia Mungatana atamzalishia Sh76 milioni aambiwa hana hatia

Mganga wa Chad aliyeambia Mungatana atamzalishia Sh76 milioni aambiwa hana hatia

Na RICHARD MUNGUTI

MGANGA aliyeshtakiwa kumlaghai Seneta wa Tana River Danson Mungatana Sh76 milioni hana hatia, hali inayoafiki msemo wa wahenga kwamba “kiendacho kwa mganga hakirudi.”

Ijapokuwa Abdoulaye Tamba Kouro aliponyoka katika shtaka la kumlaghai mwanasiasa huyo, raia huyo wa Chad alipatikana na hatia ya kupatikana pesa bandia za thamani ya Sh960,120,000.

Pia hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bw Ben Mark Ekhubi alimpata Kouro na hatia ya ulaghai wa Sh700,000.

Mganga huyo sasa amesukumwa kizimbani kujitetea kwa shtaka la kumlaghai Bw Makau Muteke $6,796 (KSh700,000) alizodai ataziwekeza katika biashara ya mafuta mnamo Machi 9, 2017.

Kouro aliyeponyoka kusukumwa jela kwa kumtapeli Bw Mungatana Sh76 milioni anazuiliwa katika Gereza la Viwandani, Nairobi.

Atakuwa anatoka mle gerezani atakapoanza kujitetea mwezi ujao.

Akimwachilia Kouro katika shtaka la kumpunja Bw Mungatana Sh76 milioni, Bw Ekhubi alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja kumhusisha mganga huyo na kosa hilo.

“Upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi kuthibitisha jinsi Bw Mungatana alivyompa Kouro mamilioni hayo ya pesa,” Bw Ekhubi alisema akitoa uamuzi ikiwa raia huyo wa Chad alikuwa na kesi ya kujibu.

“Mungatana alishindwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha alimpa Kouro mamilioni hayo ya pesa. Ilikuwa ni neno la Mungatana dhidi ya neno la Kouro,” Bw Ekhubi alisema katika uamuzi wake.

Hakimu alisema upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja ulilemaza shtaka hilo na kwamba “hana budi ila kulizamisha.”

Kouro alikuwa ameshtakiwa kumlaghai Bw Mungatana Sh76 milioni akidai ataziwekeza katika biashara ya mafuta ya petroli.

Waziri huyo msaidizi wa zamani alitapeliwa pesa hizo kati ya Aprili 20, 2011 na Aprili 29, 2013 katika mtaa wa Hurlingham Nairobi.

Alipotoa ushahidi kortini, Bw Mungatana alisema alijulishwa mshtakiwa na mtu ambaye hakufichua jina lake.

Alimkabidhi mamilioni hayo ya pesa akijifanya alikuwa na uwezo wa kuwekeza pesa hizo katika biashara ya mafuta.

Bw Mungatana alisema alianza na kumpa mshtakiwa Sh1 milioni kisha akarudishiwa zikiwa na faida.

Alimuongezea Sh5 milioni kisha akarudishiwa zikiwa na faida.

Aliongeza tena Sh10m na kurudishiwa ndipo hatimaye akampa USD ($)1,000,000 (KSh76m) ndipo Kouro alizima simu na kutoweka.

Hata hivyo, mshtakiwa alipatikana na hatia ya kuwa na pesa feki sawa na Sh960,120,000.

Kouro alipatikana na pesa bandia katika makazi yake Sandalwood katika eneo la Westlands Nairobi.

Kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki alikuwa ameomba mahakama impate na hatia mshtakiwa katika mashtaka yote.

“Nimewasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba Kouro alimtapeli Mungatana na kupatikana na pesa bandia,” alisema Bi Kariuki.

Kouro alishtakiwa kwa kughushi stakabadhi na kupatikana na pesa feki Sh9.6 milioni.

Akitamatisha ushahidi wake, Mungatana aliomba mahakama imsukumie Kouro kifungo cha miaka mingi gerezani kwa vile alimlaghai kitita kikubwa cha pesa.

Bw Mungatana aliambia mahakama aliuza magari na mali nyinginezo kumpelekea Kouro pesa hizo azieke katika biashara ya mafuta.

“Huyu Kouro amewatapeli watu wengi miongoni mwao watu mashuhuri waliogopa kujitokeza kuungama jinsi walifyoza mamilioni ya pesa,” Bw Mungatana alitoboa siri.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kupokea malalamishi ya wagonjwa moja kwa moja...

Gaspo Women walenga kuharibu mwanzo mzuri wa Vihiga Queens

T L