• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Mhubiri akiri kuiba mbuzi

Mhubiri akiri kuiba mbuzi

NA TITUS OMINDE

MWANAMUME ambaye amesema ni mchungaji wa kanisa la Israel amekiri kuiba mbuzi wanne mbele ya hakimu wa mahakama ya Eldoret.

Timona Keya ambaye alifikishwa mbele ya hakimu mkazi Tabitha Mbogua mnamo Alhamisi amekiri mashtaka ya kuiba mbuzi wanne.

Licha ya kukiri mashtaka hayo Bw Keya ambaye amefika kortini huku amevalia kitani kuonyesha kuwa yeye ni mfuasi sugu wa dhehebu la Israel -Kenya ameambia mahakama kuwa yeye ndiye alionekana na mbuzi hao mara ya mwisho kabla ya kupotea hivyo basi alikuwa tayari kulipa mlalamishi.

Mahakama imeambiwa kuwa mnamo Juni 23 katika kijiji cha Konoiyia, kaunti ndogo ya Turbo, aliiba mbuzi wanne mali ya Bw Ronald Rono.

Mbuzi hao ni wa thamani ya Sh33,000.

Mchungaji huyo ameeleza mahakama kuwa aliokoa mbuzi hao baadaye wakapotea wakiwa mikononi mwake hivyo basi hakuwa na budi ila kukiri mashtaka.

“Kama mtumishi wa Mungu niko tayari kushauriana na mlalamishi kuhusu namna nitakavyomlipa mbuzi wake,” aliambia mahakama.

Hakimu amemtaka kutangaza msimamo iwapo aliiba mbuzi husika au anasingiziwa.

Akijitetea amesema yuko tayari kubeba msalaba huo ikizingatiwa kuwa alionekana akiwa na mbuzi hao kabla ya kuripotiwa kupotea.

“Mimi ni mtumishi wa Mungu na singependa kupotezea korti muda, nilipatikana na mbuzi hao na niko tayari kulipa mlalamishi kwa awamu,” pasta Keya ameambia mahakama.

Kutokana na utatanishi wake kuhusu mashtaka hayo, mahakama imemwachilia kwa dhamana ya Sh50 au pesa taslimu Sh20 kabla ya kusomewa maelezo ya mashtaka.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Julai 3 ili mahakama itoe mwelekeo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Mtalii kutoka Ethiopia ajitia kitanzi baada ya kukosana na...

Hatua ya Ruto kuruhusu washauri watatu kwenye Baraza la...

T L