• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Hatua ya Ruto kuruhusu washauri watatu kwenye Baraza la Mawaziri yaibua maswali

Hatua ya Ruto kuruhusu washauri watatu kwenye Baraza la Mawaziri yaibua maswali

NA BENSON MATHEKA

HATUA ya Rais William Ruto kuruhusu washauri wake watatu na Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri imezua maswali kuhusu iwapo alivuka mpaka uliowekwa na Katiba.

Mnamo Jumatano, Bw Malala na washauri wa rais, Dkt David Ndii (Uchumi) Bi Monica Juma (Usalama) na Harriet Chiggai (Masuala ya Wanawake) waliapishwa kuweka siri za Baraza la Mawaziri wanavyofanya mawaziri.

Hii ni licha ya kuwa, Mahakama Kuu ilibatilisha uteuzi sawa na huo uliofanywa na mtangulizi wake Rais Ruto, Uhuru Kenyatta mnamo 2021.

Alipoteua watu 22 katika Baraza lake la Mawaziri, Rais Ruto alisema nyadhifa za Bi Juma na Bi Chiggai zilikuwa za kiwango cha uwaziri.

Hata hivyo, mawakili wanasema Katiba inafafanua kuhusu mchakato wa kuteua wanachama wa Baraza la Mawaziri na idadi yao. Ibara 152 ya Katiba ya Kenya 2010 inasema, mawaziri hawafai kupungua 14 na kuzidi 22 na kwamba, rais atawateua wakiidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

“Hatua yoyote inayokiuka katiba na mchakato uliowekwa kikatiba inazua maswali,” asema wakili Tom Maosa.

Anasema kuapishwa kwao ni ukiukaji wa katiba japo wanaweza kualikwa kutoa ushauri. Mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema, hatua ya Rais ni kutumia njia za mkato kuongeza wanachama wa Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo, anasema kuapishwa kwa wanne hao hakuwafanyi kuwa mawaziri. Taarifa kutoka Ikulu ilisema kwamba, Rais Ruto aliruhusu Bi Chiggai kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri ili kupatia umuhimu zaidi masuala ya wanawake katika utawala wake.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikuelezea sababu za kuwaruhusu Bw Malala, Bw Ndii na Bi Juma katika Baraza la Mawaziri.

Wakili Ahmednassir Abdullahi alihoji iwapo kiongozi wa nchi alifahamishwa kuhusu uamuzi wa Mahakama uliomzuia aliyekuwa Mkurugenzi wa iliyokuwa Idara ya Huduma za Nairobi Meja Jenerali Mohamed Badi kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri baada ya kuruhusiwa na Rais Kenyatta kupitia amri ya rais.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Antony Mrima katika kesi iliyowasilishwa na Bi Alice Wahome, Waziri wa Maji katika serikali ya Rais Ruto.

“Je, Mwanasheria Mkuu Mheshimwa Justin Muturi au waziri Mheshimiwa Wahome walimfahamisha Rais William Ruto kuhusu uamuzi huu wa Mahakama Kuu unaozuia wageni kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri?” alihoji Bw Abdullahi katika ujumbe wa Twitter.

Bi Wahome alikuwa mshirika wa Rais Ruto (aliyekuwa Makamu Rais) alipowasilisha kesi kupinga uamuzi wa Rais Kenyatta akisema kuruhusu Bw Badi kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri kulikiuka katiba. Katika uamuzi wake, Jaji Mrima alikubaliana na Bi Wahome kwamba, uamuzi wa Rais Kenyatta haukuidhinishwa na Bunge la Taifa.

Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alikuwa Spika wa Bunge la Kitaifa wakati uamuzi huo ulitolewa Septemba 2021.

Jaji Mrima alitoa agizo kumzuia Meja Jenerali Badi kuhudhuria mkutano wowote wa Baraza la Mawaziri, kamati za Baraza la Mawaziri au kutekeleza jukumu lolote la uwaziri. Katika kesi yake, Bi Wahome alilalamika kuwa, uamuzi wa Rais Kenyatta ulikuwa sawa na kuruhusu mgeni kuhudhuria mkutano wa baraza kuu zaidi la kufanya maamuzi ya nchi na kwa kufanya hivyo, Rais alikuwa amekiuka Katiba.

Katika uamuzi wake, Jaji Mrima alisema kwamba, wadhifa, jukumu na mamlaka ya Mkurugenzi wa NMS katika Baraza la Mawaziri halikujulikana au washtakiwa (Mwanasheria Mkuu, Katibu wa Baraza la Mawaziri na Meja Jenerali Badi) walichagua kutofichua.

“Inaonekana kama uamuzi umegubikwa na usiri na kwa hivyo hauna uwazi,” Jaji alisema katika uamuzi wake.

Kwa kuwa hakuwa amepigwa msasa na Bunge la Kitaifa, Jaji Mrima alisema kuruhusiwa kwa Mkurugenzi Mkuu huyo katika Baraza la Mawaziri kulizua maswali mengi ambayo hayakuweza kujibiwa.

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri akiri kuiba mbuzi

Ofa ya Arsenal kusajili Declan Rice kwa Sh18.7 bilioni...

T L