• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Miili mingine 14 yafukuliwa katika shamba la Mackenzie

Miili mingine 14 yafukuliwa katika shamba la Mackenzie

Miili mingine 14 yafukuliwa katika shamba la Mackenzie

 

 

Na ALEX KALAMA 

MIILI 14 ya waumini wa imani potovu inayoongozwa na mhubiri tata Paul Mackenzie wa Good News International imepatikana Jumamosi, kufuatia oparesheni ya ufukuzi wa makaburi inayoendelezwa Shakahola na maafisa wa polisi Malindi.

Kulingana na taarifa ambayo imefikia meza ya Taifa Leo, miili mitano imetolewa kwenye kaburi moja lililokuwa na baba, mama na watoto watatu.

Kaburi la pili nalo, miili miwili ya watu wazima na mtoto mmoja imefukuliwa.

Kaburi lingine lilikuwa na mtu mzima, na la nne na tano likifukuliwa mtoto na watu wanne wazima, mtawalia.

Zoezi hilo ambalo Jumamosi liliingia siku ya pili, linaongozwa na mkurugenzi wa kitengo maalum cha masuala ya mauaji Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) Bw Martin Nyuguto katika shamba la Bw Mackenzie Kijiji cha Bethlehemu, Shakahola.

Mnamo Ijumaa, miili saba ilifukuliwa katika makaburi manne.

Kufuatia uchunguzi wa polisi, huenda kukawa na makaburi mengi yaliyozikwa wafuasi wa mhubiri huyo ambaye kwa sasa anazuiliwa na askari.

Mackenzie, aidha anatuhumiwa kushawishi waumini wake kufunga bila kula wala kunywa maji, akiwahadaa kwamba wakifa watakutana na Yesu.

Kando na miili iliyofukuliwa Ijumaa na Jumamosi, visa kadha vya maafa ya njaa yanayohusishwa na hadaa za pasta huyo pia vameandikishwa.

Alikamatwa Aprili 15 na kusukumwa kortini siku mbili baadaye, mahakama ikiamuru azuiliwe kwa muda wa siku 14 kuruhusu polisi kufanya uchunguzi.

Wakati huohuo, Taifa Leo imearifiwa kwamba Mackenzie amekuwa na wake wanne, watatu ikisemekana walifariki awali katika hali isiyoeleweka.

Mhubiri Mackenzie akiingizwa seli. Picha / ALEX KALAMA

Wote, duru zinaarifu wamekuwa wafuasi wa dini yake.

Mwaka 2019, pasta huyo alikamatwa na kuachiliwa huru na mahakama kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi wa kutosha, akituhumiwa kupotosha waumini wake.

Ufukuaji wa makaburi bado unaendelea katika Msitu wa Shakahola.

Mackenzie naye, amesusia kula akiambia maafisa wa polisi kwamba yuko kwenye mfungo.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ukimwi: Idadi ya maambukizi mapya yapungua Siaya

Machafuko Sudan yasababisha changamoto kubwa za kibinadamu

T L