• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:00 PM
Murkomen amshtaki Cherargei vita vya ubabe Bonde la Ufa vikichacha

Murkomen amshtaki Cherargei vita vya ubabe Bonde la Ufa vikichacha

NA VITALIS KIMUTAI

MVUTANO mkali wa ubabe unatokota katika ngome ya Rais William Ruto ya Bonde la Ufa huku Waziri wa Uchukuzi, Kipchumba Murkomen, akitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Seneta wa Nandi, Simon Cherargei, akimlaumu kwa kumharibia jina.

Hatua hii inajiri huku baadhi ya wabunge wakilaumu mawaziri, akiwemo Murkomen, kwa kudhaniwa kutofanya kazi vizuri na kuingilia siasa za mashinani, zinazohusishwa na siasa za urithi za 2032.

Kupitia kampuni ya mawakili ya Ongoya na Wambola Advocates, Waziri Murkomen anataka Seneta Cherargei kumuomba msamaha kufuatia matamshi aliyotoa Novemba 29, akidai yalimchafulia jina.

Barua hiyo inadai kwamba Bw Cherargei alimsawiri Murkomen kama mfisadi, aliyepokea hongo, kukosa uadilifu, msaliti wa wapigakura na kiongozi asiyefaa kushikilia afisi ya umma.

Kupitia kampuni hiyo ya mawakili, Murkomen alisema kwamba anachukulia matamshi ya Seneta Cherargei kama ya kumharibia sifa. 
Bw Cherargei, hata hivyo, amesema kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba hataomba msamaha na yuko tayari kukabiliana na suala hilo mahakamani.

Mzozo huu wa kisheria unaongeza mzozo unaoendelea kati ya Waziri Murkomen na kundi la wabunge na magavana kutoka Bonde la Ufa, unaohusu ugawaji wa rasilimali na mvutano wa mamlaka unaohusishwa na siasa za urithi za 2032.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Bw Cherargei alisema hatua ya wabunge kuchunguza waziri ni wajibu wao wa kuhakikisha utawala bora.

“Hakuna chochote cha kibinafsi katika kuwafanya mawaziri kuwajibika. Kwa kweli, ikiwa mawaziri watashindwa katika kazi zao, inamaanisha rais ameshindwa. Hatutaki hilo lifanyike chini ya uangalizi wetu,” Bw Cherargei aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

“Je, kuna nini cha kibinafsi, kwa mfano, kumuuliza Bw Murkomen ni kwa nini Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta ulikuwa katika hali mbaya kwa sababu paa zinavuja na hilo ni jambo ambalo limeaibisha nchi yetu? Kwa nini mtu aunde kamati ya kuchunguza hilo? Tunapouliza kuhusu hali ya barabara na viwanja vya ndege, ni suala la kibinafsi au la kitaifa?” Bw Cherargei alihoji.

Kundi la viongozi akiwemo Gavana wa Bomet, Hillary Barchok, Mwakilishi wa Wanawake wa Nandi, Cynthia Muge na Cherargei, wamelaumu Bw Murkomen kwa kuingilia siasa za maeneo ya Kusini na Kaskazini mwa Bonde la Ufa huku wakidai amenyima baadhi ya kaunti pesa za ujenzi wa barabara.

Mbunge wa Emurua Dikirr, Johana Ng’eno, amezidisha mvutano kwa kutaka kuwa msemaji wa Bonde la Ufa, na kumvuta waziri katika siasa za urithi mnamo 2032.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea, Arsenal na Man-Utd ni vichapo tu!

Azimio yaendelea kupasuka Wamalwa sasa akitofautiana na...

T L