• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Azimio yaendelea kupasuka Wamalwa sasa akitofautiana na Raila

Azimio yaendelea kupasuka Wamalwa sasa akitofautiana na Raila

Na JUSTUS OCHIENG

MIGAWANYIKO inaendelea kukumba muungano wa Azimio la Umoja One Kenya huku mmoja wa vinara Eugene Wamalwa akipinga pendekezo la kiongozi wa ODM Raila Odinga la kuandaliwa kwa kura ya maamuzi nchini.

Bw Wamalwa ambaye alikuwa mwanachama wa Kamati ya Maridhiano (NADCO), amejitokeza kupinga ripoti hiyo akisema haikugusia suala la kupunguzwa kwa gharama ya maisha.

Bw Odinga amenukuliwa akisema kura ya maamuzi inastahili kuandaliwa Wakenya waamue iwapo wanataka kubuniwe Afisi ya Kiongozi wa Upinzani pamoja na wadhifa wa Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Bw Wamalwa Jumapili aliambia Taifa Leo kuwa haitakuwa haki iwapo Wakenya watatakiwa washiriki kura ya maamuzi ilhali wanahangaishwa na gharama juu ya maisha.

Baada ya kukataa kuidhinisha ripoti ya Nadco na hata kukataa marupurupu, Bw Wamalwa sasa anaonekana yuko tayari kukabiliana na Bw Odinga na vinara wengine wanaounga mkono ripoti hiyo.

Kinara wa Narc Kenya, Martha Karua, pia amenukuliwa akipinga ripoti ya Nadco, viongozi hao wawili sasa wakionekana kuzua misukosuko ndani ya Azimio.

“Bila suala la kushushwa kwa gharama ya maisha kushughulikiwa, hatutaunga mkono kura ya maamuzi na hiyo ndiyo maana mimi sijatia saini ripoti hiyo,” akasema Bw Wamalwa.

“Hata Wakenya wenyewe hawataunga mkono kura hiyo ya maamuzi,” akaongeza.

Alikariri kuwa kwa sasa Wakenya wanaumia kiuchumi na wamesakamwa na njaa pamoja na kulemewa na uzito wa kutimizia familia zao masuala ya kimsingi kama karo na chakula.

Bi Karua amekuwa akikashifu ripoti hiyo na kusema kuwa ni ‘hadaa tupu’ ambayo inastahili kupingwa na Wakenya. Kamati ya Nadco ilikuwa ikiongozwa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aliyewakilisha Azimio pamoja na Kiongozi wa Wengi Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah.

Mnamo Alhamisi, Desemba 7, 2023, Bi Karua alitofautiana na Bw Odinga kuhusiana na ripoti ya Nadco na akatoa wito ipingwe na Wakenya wote.

“Ripoti ya Nadco haina chochote cha kumnusuru mwananchi wa kawaida ila inabuni vyeo kwa viongozi. Ni ukora ambao Wakenya wanastahili kuukataa kabisa,” akasema Bi Karua.

Hoja kuwa Bw Wamalwa na Bi Karua wanapinga ripoti hiyo imeibua madai kuhusu hatima ya Azimio, vinara wake wakiendelea kuvutia pande tofauti.

Ingawa hivyo, waziri huyo wa zamani alikanusha kuwa kuna mgawanyiko akisema kuwa kuna uhuru wa kuzungumza kuhusu suala hilo muhimu kitaifa.

“Azimio ni vuguvugu linalozingatia demokrasia na kuruhusu maoni kinzani. Watu hawafai kujifasiria kuwa kuna mgawanyiko au kuwa na wasiwasi wangu wa kukataa kutia saini ripoti ya Nadco,” akasema Bw Wamalwa.

  • Tags

You can share this post!

Murkomen amshtaki Cherargei vita vya ubabe Bonde la Ufa...

Mwanasoka wa zamani wa Harambee Stars, Ahmed Breik aaga...

T L