• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Mwanafunzi aliyemuua mwenzake kwa kisu akamatwa Lamu

Mwanafunzi aliyemuua mwenzake kwa kisu akamatwa Lamu

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa polisi wamemtia mbaroni mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Upili ya Faza iliyoko Lamu ambaye alimuua kwa kumdunga kisu mwenzake wa Kidato cha Nne.

Kamanda wa Polisi wa Lamu William Samoei amethibitisha leo Alhamisi kwamba mwanafunzi Mohammed Idarus Mohammed, alikamatwa akiwa mafichoni katika kijiji cha Tchundwa.

Anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kizingitini, Lamu Mashariki kusubiri kupelekwa mahakamani wakati wowote kutoka sasa.

Mwanafunzi Mohamed Bakari aliyeuawa na Idarus mnamo Jumatatu alizikwa katika mazishi yaliyojaa majonzi na masikitiko.

Mwanafunzi huyo aliuawa majira ya asubuhi pale alipokuwa ametembelea rafikiye wa Kidato cha Tatu kabla ya kuvamiwa na mmoja wa wanafunzi na kumdunga kisu kwa nyuma na kumuua papo hapo kabla ya kutoroka.

Hali ya huzuni ilitanda Jumatatu jioni wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye maziara ya Faza waombolezaji wakimtaja mwendazake kuwa mwanafunzi mpole na mwenye bidii.

Miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni mwalimu mkuu wa shule ya Upili ya Faza, Hannington Shoka, Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Lamu, Joshua Kaaga, maafisa wa elimu wa Lamu Mashariki na walinda usalama waliohakikisha kuna ulinzi mkali wakati wa shughuli hiyo ya mazishi.

Mauaji ya mwanafunzi huyo yalizua uhasama kati ya kijiji cha Faza ambapo marehemu anatoka na kile jirani cha Tchundwa ambacho mwanafunzi muuaji anatoka.

Jumatatu, muda mfupi baada ya mauaji hayo, wakazi wa vijiji hivyo viwili walikabiliana vikali, hali iliyozua taharuki kwenye vijiji husika, hivyo kulazimu polisi kuingilia kati na kutuliza ghasia.

Mwanachama wa Bodi ya Elimu na Utawala (B.O.M) shuleni Faza, Mohamed Ali, aliiomba idara ya usalama kuchunguza kwa kina tukio hilo la mauaji ya kushangaza na kuhakikisha mhalifu amechukuliwa hatua kali za kisheria ili familia ya mwendazake ipate haki.

“Tayari taharuki ipo kutokana na kwamba mshukiwa ametoroka na kujificha. Ni vyema jamii ya Faza na Tchundwa kushirikiana vilivyo. Wacha mwanafunzi muuaji atolewe na kukabidhiwa polisi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake. Kuendelea kumficha mhalifu kunaleta uhasama na tofauti zaidi zisizofaa,” akasema Bw Ali.

Bi Fatma Aboud alikashifu kitendo cha mwanafunzi kujiohami kwa kisu na kumuua mwenzake, akitaja kuwa tukio hilo linadhihirisha jinsi hali ya nidhamu kwa wanafunzi wa Lamu Mashariki ilivyodorora.

“Ninafahamishwa kuwa mwanafunzi aliyeua mwenzake hata hakuwa ameripoti shuleni tangu muhula wa pili ulipoanza. Yaani alifika shuleni Jumatatu kuja kutekeleza mauaji na kisha kutoweka. Huo ni ukosefu mkubwa wa nidhamu na lazima tukio hili lishughulikiwe vilivyo ili liwe funzo kwa wengine.

Mauaji ya mwanafunzi huyo kwa kudungwa kisu yanajiri wakati ambapo kuna marufuku ya kutobeba au kujihami kwa silaha yoyote, ikiwemo visu, mapanga na marungu kwenye maeneo ya umma kote Lamu.

Sheria hiyo ilitangazwa na idara ya usalama ya kaunti ya Lamu tangu 2015 baada ya visa vya mauaji kupitia visu na mapanga kukithiri kote Lamu.

  • Tags

You can share this post!

ULIMBWENDE: Ili usiwe na chunusi, epuka vyakula hivi

Waiguru alaumiwa kwa kuachilia kampuni ya maji ya Kirinyaga...

T L