• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Waiguru alaumiwa kwa kuachilia kampuni ya maji ya Kirinyaga kupata hasara

Waiguru alaumiwa kwa kuachilia kampuni ya maji ya Kirinyaga kupata hasara

NA CHARLES WASONGA

MASENETA mnamo Jumatano, Mei 17, 2023 walimlaumu Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kwa kutofuatilia kwa makini utendakazi wa Kampuni ya Maji Kirinyaga (KIWASCO) hali ambayo imesababisha kampuni hiyo kupoteza maji ya thamani ya Sh407 milioni.

Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021, maji hayo ni sawa na asimilia 60 ya lita 4.5 milioni za maji yaliyozalishwa na kampuni hiyo katika mwaka huo.

“Ikiwa asilimia 60 ya maji yaliyozalishwa na kampuni hii hayakulipiwa wakati huo hii ina maana kuwa kampuni hii ilipata hasara ya Sh407 milioni, ambayo ndio thamani ya maji hayo,” akasema mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uwezekazaji na Hazina za Kipekee Godfrey Osotsi.

Bw Osotsi, ambaye ni seneta wa Vihiga, alisema kulingana na sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Huduma za Maji (WASREB) kampuni za maji zinafaa kulipia angalau asilimia 75 ya maji ambayo zinazalisha kila mwaka.

“Endapo Serikali ya Kaunti ya Kirinyaga ingekuwa ikifuatilia kwa makini utendakazi wa kampuni hii ya Kiwasco basi hasara kama hii haingetokea na kampuni hii iweza kupata faida kubwa zaidi kuliko faidi ya Sh50 milioni inayotajwa hapa,” akasema.

Awali, Bi Waiguru ambaye alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kujibu masuala yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, alisema kuwa serikali yake sio mwenye hisa katika kampuni hiyo ya maji ya Kiwasco.

“Kampuni hii inaendeshwa kwa njia huru chini ya usimamizi wa Bodi ya Wakurugenzi. Serikali yangu sio mwenye hisa katika kampuni licha kwa kwamba Katibu wa Kaunti ni mwanachama wa Bodi ya Usimamizi,” akasema Gavana huyo ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (CoG).

Kauli yake ilipingwa vikali na Bw Osotsi aliyeungwa mkono na wanachama wa kamati hiyo Karungo Wa Thang’wa (Kiambu), Eddy Oketch (Migori) na Seneta Maalum Miraj Abdallah.

  • Tags

You can share this post!

Mwanafunzi aliyemuua mwenzake kwa kisu akamatwa Lamu

Fahamu kwa nini unapaswa kula dengu mara kwa mara

T L