• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Mwanamume aliyebeba maiti ya mkewe hadi kituoni ageuka mshukiwa mkuu

Mwanamume aliyebeba maiti ya mkewe hadi kituoni ageuka mshukiwa mkuu

NA MWANGI MUIRURI 

MWANAMUME mmoja wa Murang’a ametiwa mbaroni kwa madai kwamba alimuua mke wake usiku wa Agosti 19, 2023, katika kisa kinachodaiwa ni mzozo wa bangi ya Sh3,000.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Maragua Bw Joshua Okello, mshukiwa alibeba maiti ya mkewe hadi katika kituo cha polisi na kudai alimwokota kutoka shamba la migomba ya ndizi.

“Alifika katika stesheni ya Maragua akidai kwamba mwanamke huyo alikuwa mlevi na alikuwa ameaga dunia,” akasema.

Bw Okello alisema kwamba maafisa wa polisi waliingiwa na shaka lakini wakampa mwanamume huyo barua ya kuwasilisha mwili katika mochari ya Murang’a.

“Uchunguzi ulipokuwa ukiendelea, wakazi wa mtaa wa Mathare waliandamana wakidai kuwa maafisa wa polisi walikuwa wakisaidia mwanamume huyo kuficha ukweli,” akasema Bw Okello.

Hali iliishia mwanamume huyo kutiwa mbaroni mnamo Jumatatu, Agosti 21, 2023, na ambapo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Maragua.

“Kwa sasa tunasubiri ripoti ya upasuaji maiti ndipo ibainike mazingara halisi ambapo aliaga dunia. Kuna majirani ambao wanasema walishuhudia mwanamume huyo akimshambulia mwendazake kwa msingi wa kuuza bangi ya Sh3,000,” akasema.

Bw Okello alisema kwamba “taarifa hizo zote zitaandikishwa rasmi ili kuupa uchunguzi mwelekeo”.

Bw Okello alisema kwamba “maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wameanza kufanya uchunguzi wa kina na iwapo mwanamume huyo atahusishwa na mauaji ya mkewe, atashtakiwa”.

  • Tags

You can share this post!

‘Kufumbia macho maadili ya Kiafrika ni kuendeleza...

Udukuzi wa e-Citizen waletea Wakenya nafasi 250 za kazi

T L