• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:07 PM
Mwanamume mpenda sketi ashtakiwa kwa ubakaji

Mwanamume mpenda sketi ashtakiwa kwa ubakaji

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA moja ya Nairobi imeombwa imzuilie gerezani mwanaume anayeishi katika mtaa unaoishi maafisa wakuu wa Kijeshi (KDF) kwa madai ni “hatari kwa usalama kwa wasichana wa vyuo vikuu na wale wa umri mdogo.”

Hakimu mwandamizi Bi Esther Boke alielezwa Abdirizak Adan Abdullahi, “yuko na shauku ya hali ya juu na hamu isiyoridhika ya kuwapepeta wasichana huku amewashikia bastola vichwani.”

Kiongozi wa mashtaka Allan Mogere alipinga vikali Abdullahi akiachiliwa kwa dhamana akisema “ni hatari kwa usalama wa kitaifa na pia kwa wasichana wa vyuo vikuu na wale walio balehe.”

Bw Mogere alisema mshtakiwa anamiliki bastola licha ya kwamba polisi wameisaka pasi mafanikio lakini baadhi ya walalamishi waliopiga ripoti kwa polisi wameeleza “ walitishwa na bastola na mshtakiwa wakikataa kuitikia vishawishi vyake.”

Pia korti ilielezwa mshtakiwa anaishi katika mtaa uliokodishiwa maafisa wakuu wa kijeshi na ni vigumu polisi kuingia mle kumsaka mshtakiwa endapo ataachiliwa kwa dhamana.

“Abdullahi na mshtakiwa mwenzake Faith Washiali Bwibo wako na ushawishi mkubwa na licha ya kwamba kuna Lokodaoni wanaweza kutoroka endapo wataachiliwa kwa dhamana,” alisema Bw Mogere,

Vile vile wakili Amazon Koech anayemwakilisha mhasiriwa alisisitiza , “ Abdullahi huyu hana utu.Alimbaka mlalamishi katika mtaa wa Mugoya ulioko eneo la South C kaunti ya Nairobi. Pia akimtumia Faith Washiali Bwibo alimsaliti na kumpeleka mlalamishi tena eneo duni kaunti ndogo ya Naivasha ambapo alimtupa kwenye jangwa usiku aliwe na Wanyama mwitu baada ya kukataa akimdhulumu kimapenzi.”

Bi Koech alisema Abdullahi hana huruma hata kwa vile ameripotiwa katika kituo cha Polisi cha Langata kwamba “ amewabaka wasichana wengine sita lakini akawatisha na bastola kusudi asishtakiwe.”

Wakili huyo akitegemea taarifa ya kiapo ya afisa anayechunguza kesi hiyo Koplo Peris Makio Mghanga, alisema , “ wasichana kadha wanatazamiwa kufika kortini kusimulia yaliyowakumba wakiwa mikononi mwa Abdullahi.”

“Wasichana waliokataa kumfurahisha kimapenzi mshtakiwa walipata kichapo cha mbwa na nguruwe nusra wachomwe kwa maji moto kisha wanatupwa nje usiku wa manane,” Bi Koech alidokeza.

Wakili huyo aliyesheheni katika kuwatetea kina mama na wasichana wanaodhulumiwa kimapenzi aliomba korti “iwe na moyo wa huruma na kukataa kuwaachilia Abdullahi na Faith aliosem wanashirikiana kuwadhulumu wasichana wa umri mdogo kimapenzi.”

Mahakama ilielezwa mlalamishi ni mwanafunzi anayefanya shahada ya digrii ya uanasheria ni bintiye wakili mwenye tajriba ya juu jijini Nairobi.

Mnamo Machi 20, 2021 , Faith ambaye ni rafikiye mlalamishi alimshawishi wakutane katika kituo kimoja cha kuuza mafuta ya Petroli alipwe simu yake muundo wa IPhone yenye thamani ya Sh40,000 iliyokuwa imeharibiwa na Abdullahi siku ile alibakwa.

Badala ya kulipwa simu, Faith , Abdullahi na mlalamishi walifufuliza hadi Naivasha ambapo washtakiwa walikodisha chumba na kumtaka mlalamishi ashiriki tendo la ngono.Alikataa na usiku huo alitupwa nje gizani aliwe na Wanyama mwitu.

Mlalamishi pamoja na wasichana wengine waliokataa vishawishi vya mshtakiwa walikutwa na polisi na kuokolewa.

Koplo Mghanga ameeleza mahakama Abdullahi alitambuliwa na mlalamishi katika kituo cha polisi cha Langata kuwa ndiye aliyemdhulumu kimapenzi.

Lakini wakili anayewatetea Abdullahi na Faith alipinga ombi hilo la kuwanyima washtakiwa dhamana akisema , “ Kifungu nambari 49 cha katiba chaamuru kila mshukiwa aachiliwe kwa dhamana hata kama anakabiliwa na kesi ya aina gani.”

Alipinga hatua ya Bw Mogere kusema washtakiwa wanyimwe haki yao.

Pia wakili huyo aliteta kwamba “hakupewa nakala ya taarifa ya kiapo ya Koplo Mghanga kwa wakati unaofaa kupata maelezo ya washtakiwa kuhusu madai yao.”

“Je unataka muda kujibu madai ya upande wa mashtaka na mawakili wa mhasiriwa,” Bi Boke alimwuliza wakili huyo wa washtakiwa mara mbili.

“Hapana sitaki muda.Naomba korti isajili kwamba sikupewa nakala ya ushahidi wa Koplo Mghanga kwa wakati unaofaa,” alijibu wakili huyo ambaye hakutaka jina lake lichapishwe.

Hakimu aliamuru washtakiwa wazuiliwe hadi Aprili 9, 2021 atakapotoa mwelekeo.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool ni muujiza tu sasa UEFA ila Zidane asema kazi...

Siku mbili zatenganisha kifo cha mwanamuziki Albert Gacheru...