• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Mwili wa mwanamume wapatikana ukining’inia nyumbani South B

Mwili wa mwanamume wapatikana ukining’inia nyumbani South B

MAAFISA wa polisi katika eneo la Makadara wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamume ulipatikana ukining’inia katika paa la nyumba ya mamake mwishoni mwa wiki.

Kamanda wa polisi kwenye eneo hilo, Bw Timon Odingo alisema kisa hicho kilitokea mwendo wa usiku katika eneo la Crescent, mtaani wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba ulioko South B.

Aidha, Bw Odingo aliongeza kwamba mwili wa marehemu, Bw James Mutie, 30 ulipatikana ndani ya nyumba ya mamake mzazi ukining’inia kutoka paa la nyumba.

“Mwili wa Bw James Mutie ulipatikana ukining’inia kutoka paa la nyumba ya mamake. Hakuna ujumbe wowote ulipatikana umeandikwa na marehemu wala hakuna taarifa ya chanzo cha tukio hilo japo makachero wameanzisha uchunguzi wao,” Bw Odingo akaongeza.

Zaidi ya hayo ni kwamba wakazi katika mtaa huo waliambia Taifa Leo kwamba marehemu alidaiwa kuanza vituko nyakati za mchana.

Awali, inadaiwa marehemu alionekana amechomoka mtaani akibeba kisu ambacho alijidunga nacho mwilini akitaka kujiua.

“Alionekana akishika kisu mkononi na alijidunga mara kadhaa mwilini akikimbia kuelekea barabarani ya Entreprise kabla ya marafiki wake wa karibu kumtuliza,” Bw mmoja aliyeomba asitajwe jina akanena.

Duru zilieleza kwamba baadaye alipelekwa katika hospitali moja katika maeneo ya Eastlands jijini Nairobi pale daktari aliwashauri waliompeleka hospitalini wawe karibu naye kwani alipatikana akiwa na msongo wa mawazo.

“Ushauri wa daktari ulikuwa watu wasimwache peke yake kutokana na msongo wa mawazo uliomkumba,” mama mmoja akasema.

Mwanamume mwingine kutoka familia ya marehemu aliongeza kwamba kisanga hicho kilitokea wakati babake marehemu alipokuwa amelazwa hospitalini akitibiwa.

Vilevile, mamake marehemu alilazimika kuwacha babake kwenye kitanda cha wodi akimbie mtaani kuona mwanawe baada ya kupashwa kuhusu visanga vya mtoto wake.

“Kinachotuweka huzuni ni kwamba marehemu ndiye mwanamume wa pekee katika watoto wengine ambao ni wasichana tupu wa familia yao,” mwanamke aliyejitambulisha kwa jina moja Bi Penninah akanena.

Marehemu alikuwa akifanya kazi ya juakali akihusishwa na biashara ya kununua na kuuza vyuma kuukuu.

Wanomjua walisema alikuwa mcheshi, mtulivu na mwenye kutangamana na watu.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wakenya hawajaona zawadi ya stima nafuu

WANTO WARUI: Walimu wana kibarua kuandaa watahiniwa kwa...

T L