• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 AM
TAHARIRI: Wakenya hawajaona zawadi ya stima nafuu

TAHARIRI: Wakenya hawajaona zawadi ya stima nafuu

Na MHARIRI

HUKU Wakenya wakimaliziamalizia sherehe za Krismasi wikendi iliyoisha, wengi wamegutuka kutambua kwamba ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu stima nafuu haikutimia.

Wengi walioenda kulipia stima haswa katika ule mfumo wa prepaid walipigwa na butwaa kuona kwamba stima ingali juu ajabu.

Mara ya kwanza Rais alipotoa ahadi hiyo, alisema kwamba jopo jipya aliloteua likiongozwa na John Ngumi lingekaa chini na kutathmini jinsi stima itapunguzwa kwa asili mia 30 kufikia Krismasi mwaka huu.

Lakini kufikia Novemba, jopo hilo liliripoti kwamba mojawapo ya vizingi vikubwa katika kushukisha bei ya stima ni ile mikataba ya wazalishaji umeme, almaarufu Indipendent Power Producers Aggrements (IPPAs)ambayo inauzia kampuni ya Kenya Power umeme kwa bei ya juu mno hata kushinda shirika la kitaifa la KenGen, mbali na ushuru mkubwa uliochangia hadi asili mia 5o ya bili ya stima.

Kufikia mapema Desemba, ilikuwa wazi kwamba ahadi ya kupunguza bili za stima kwa asili mia 30 haingetimia na hapo Rais Kenyatta katika hotuba yake ya Jamhuri Dei akasema kwamba stima itapunguzwa kwa mgao: asili mia 15 kufikia Krismasi na asili mia hiyo nyingine ya 15 kufikia Machi 2022.

Akasema kwamba vichocheo vitakavyosaidia kupungua huko ni mikakati ya kuondoa ubadhirifu na miundo mibovu inayofanya umeme kupotea bure.

Lakini ni wazi kwamba ahadi hiyo haijatimia haswa kwa wale ambao wananunua salio (tokens). Kwa mfano, mteja aliyetumia Sh1,500 kununua salio ya stima, alipokea chache hata kuliko vile ilivyokuwa Novemba.

Kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari, ni kwamba hata licha ya kukabili mianya ambayo inapoteza stima na kufanya bei kusalia juu, kizingiti kikuu kingali kinasalia hili suala la mikataba na mashirika yanayouzia Kenya Powert stima.

Kubadili mikataba hiyo ni kizungumkuti. Baadhi ya mikataba hiyo ina muda wa hadi miaka 20. Na mikataba hiyo ina vipengele vigumu mno kiasi kwamba hata wakati shirika la kitaifa KenGen linapozalisha umeme nafuu, lazima Kenya Power inajikuta ikinunua stima kutoka kwa wenye IPPs.

Hivyo basi, huku serikali ikijikuna kichwa jinsi gani suala hili la mikataba ghali litakabiliwa na kuleta mwamko mpya wa stima nafuu kwa wafanyabiashara, wenye viwanda na watumiaji wa kawaida nyumbani, ukweli unaobakia ni kwamba umeme ungali ghali mno.

Na Rais Kenyatta yupo hatarini kuonekana kwamba asiyetimiza ahadi na ni jukumu lake kutumia mamlaka yote aliyo nayo kikatiba kuletea wananachi wa kawaida afueni.

You can share this post!

Wakenya washerehekea Krismasi sehemu mbalimbali

Mwili wa mwanamume wapatikana ukining’inia nyumbani...

T L