• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 11:13 AM
Nani anameza wanaume Pwani?

Nani anameza wanaume Pwani?

Na WAANDISHI WETU

WAKAZI wa Pwani wanaishi kwa hofu na wasiwasi mkubwa kufuatia ongezeko la visa vya wanaume kutoweka kiholela. Visa hivyo vilianza kuongezeka Kenya ilipoimarisha kampeni dhidi ya ugaidi takribani miaka 10 iliyopita.

Kulingana na familia za waathiriwa, juhudi za kutafuta usaidizi wa polisi hazijafanikiwa, hali inayozua shauku kuwa, huenda maafisa wa usalama wanahusika. Ripoti moja ya serikali ya Amerika ilitaja kutoweka kwa watu miongoni mwa matukio ya kutisha yanayokiuka haki za binadamu Kenya.

Kufikia Novemba 2020, mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo hufuatilia visa hivyo yalipokea ripoti 127 kuhusu watu waliotoweka kwa njia ya kutatanisha. Mwaka huu, Shirika la Haki Africa lilisema, jumla ya watu 26 walitoweka nchini kati ya Januari na Agosti mwaka huu, ambapo 21 ni kutoka kaunti za Pwani ilhali watano ni kutoka Nairobi.

Katika ripoti ambayo shirika hilo lilizindua Agosti wakati wa maadhimisho ya siku ya waliotoweka ulimwenguni, ilibainika Kaunti za Kwale, Mombasa na Lamu ziliongoza kwa idadi ya waliotoweka wasijulikane walipo.

Kwale inaongozwa kwa visa 10, Mombasa visa 6 ilhali Lamu ina visa vitano. Inaaminika huenda kuna visa vingine vingi ambavyo havijaripotiwa. “Nchi hii lazima ikatae kuzama kwenye ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu.

Asasi za usalama lazima zitambue kuwa heshima kwa haki za binadamu ni msingi muhimu wa kudumisha usalama,” Mkurugenzi Mkuu wa Haki Afrika, Hussein Khalid alisema wiki jana. Matamshi yake yalifuatia kisa ambapo Prof Hassan Nandwa alitoweka baada ya mhukumiwa wa ugaidi, Elgiva Bwire kutekwa nyara alipokamilisha kifungo chake cha miaka 10 gerezani. Prof Nandwa alikuwa wakili wa Bwire.

Idara ya polisi ilionekana kujitenga na kutoweka kwa Bwire wakati Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ilimworodhesha miongoni mwa washukiwa wa ugaidi wanaosakwa. Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, DCI ilidai Bwire aliapa kulipiza kisasi kwa umma na maafisa wa usalama na inaaminika alienda mafichoni kupanga mashambulio ya kigaidi.

Wengine walio katika orodha iliyotolewa ya washukiwa wa ugaidi wanaosakwa ni Barigi Abdikadir Haila kutoka Moyale, Mohammad Abubakar kutoka Mombasa, Trevor Ndwiga kutoka Nairobi na Salim Rashid Mohamed kutoka Mombasa.

Mojawapo ya visa vya watu kutoweka ambavyo viligonga vichwa vya habari Pwani mwaka huu ni kile cha Abdulhakim Salim Sagar, ambaye ilisemekana alitoweka baada ya kukamatwa na polisi kuhusu ugaidi.

Bw Sagar, ambaye alipatikana baada ya takribani mwezi mmoja kufuatia lalama za viongozi wa Kiislamu, familia yake na mashirika ya kijamii, alikuwa na kesi kuhusu madai ya ugaidi na alikuwa akiripoti kwa mpelelezi mara moja kwa mwezi.

Sawa na visa vingine vya awali, familia yake ilidai watu waliomchukua walijitambulisha kuwa ni polisi. Hata hivyo, kama sasa ilivyo desturi, polisi walikana kuhusika. “Polisi hawateki watu nyara. Wanachoweza kufanya ni kukamata watuhumiwa kufuatia ripoti zilizotolewa kwa kituo cha polisi,” Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Pwani, Bw Manase Mwania Musyoka alimwambia Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa, Anne Ong’injo akijibu kesi iliyowasilishwa na familia ya Bw Sagar, ambapo walitaka polisi walazimishwe kumsalimisha kwao.

Naye Mursal Mohammed Macharia, 25, alitoweka Septemba 28 mwaka huu katika eneo la Kiunga, Kaunti ya Lamu ambako familia yake inasema alikuwa mhudumu wa bodaboda. Kulingana na shangazi yake, Bi Faiza Famou, kijana huyo alipigiwa simu na rafiki yake ambaye ni afisa wa polisi ili wakakutane katika mkahawa ulio katika kituo cha polisi.

“Mtu huyo ambaye alituambia ni rafiki yake alimpigia simu tena mara ya pili. Mursal hakumaliza chakula alichokuwa akila, akaenda kukutana na huyo rafiki yake. Hiyo ilikuwa mara yetu ya mwisho kumwona na hadi leo, hatujasikia chochote kutoka kwake. Simu yake ilizimwa,” akaeleza, katika mahojiano ya awali.

Polisi katika kaunti hiyo walikanusha kufahamu aliko mwanamume huyo. Familia mbalimbali na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamehusisha visa vingi katika maeneo ya Pwani na vita dhidi ya ugaidi, ila katika maeneo mengine kama vile eneo la kati na Nairobi, visa aina hiyo hushukiwa kuhusiana na aina nyingine za uhalifu pamoja na migogoro ya kibiashara au kifamilia.

Familia ya mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 22 ambaye anasakwa kwa kuhusishwa na magaidi wa Al-Shabaab inataka majibu kutoka kwa serikali kuhusu aliko. Bi Zahara Mohamed alikanusha madai kwamba mwanawe, Bw Muhamad Abubakar Said ni gaidi au ana uhusiano na wanamgambo hao.

‘Mwanangu hajawahi kuwa na silaha, au kuvuka mpaka kwenda Somalia kwa sababu yoyote,’ alisema. Bi Mohamed amepuzilia mbali taarifa zinazodai mwanawe ni mmoja wa washukiwa wakuu ambao tayari serikali imetoa ahadi ya Sh10 milioni kwa atakayepeana habari kuhusu walipo.

Bw Muhamad, almaarufu Minshawary, alidaiwa kutekwa nyara mnamo Oktoba 14 katika eneo la Seven-Up, Majengo baada ya kuhudhuria sala ya Ishaa katika msikiti wa Masjid Azhar saa mbili unusu jioni. Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Umma hajaonekana tangu wakati huo. Familia yake hata hivyo imeshikilia kuwa idara ya polisi ina ufahamu kuhusu aliko.

Ripoti za Farhiya Hussein, Kalume Kazungu, Brian Ocharo na Valentine Obara

You can share this post!

Bidhaa: Maafisa walaumiwa kwa kuzembea

Pigo kwa Liverpool na Senegal fowadi tegemeo Sadio Mane...

T L