• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Papara na pupa hazileti ufanisi katika maisha

Papara na pupa hazileti ufanisi katika maisha

Na MHARIRI

LAITI mwanadamu angalikuwa msikizi na msikivu mahiri aliyemakinika katika kusikiliza kwake, hakika mafanikio mengi yangalipatikana maishani! Lakini ole wetu! Sisi wanadamu, nafsi zetu zimemilikiwa na kutamalakiwa na hulka za papara na pupa daima dawamu!

Tunasahau kwamba mwenye pupa hadiriki kula tamu; simba mwenda pole ndiye mla nyama; tamaa mbele mauti nyuma; polepole ya kobe humfikisha mbali; papo kwa papo kamba hukata jiwe na mtaka yote kwa pupa hukosa yote!!Katika dunia hii, kila mtu ni mhitaji na mtafutaji! Watu wote wanapania kusaka riziki na mahitaji muhimu ili maisha yasonge mbele! Na kwa bahati njema, kila kitu anachokihitaji mwanadamu kinapatikana papa hapa duniani.

Ukitaka chakula, pesa, mavazi, nyumba, shamba, kazi, furaha na shibe, vyote utavipata! Lakini kuna siri kubwa katika kuyapata mafanikio hayo yote tuliyoyataja. Siri yenyewe imo ndani ya uvumilivu, subira na stahamala! Hiyo ndiyo sababu watu wachache wavumiliao ndio wanaofanikiwa kuyapata mahitaji yao kwa njia halali! Watu wenye papara na pupa ni muhali kufanikiwa, chambilecho wahenga, ‘Mwenye pupa hadiriki kula tamu!’Tujifunze kuvumilia.

Tuwe na subira siku zote! Subira huvuta heri! Kila mja akitafuta kwa uvumilivu atapata! Tusitamani kuishi katika dhana za kutarajia miujiza ati kwamba ukitaka kitu, kipatikane hapo hapo! Hizo zilikuwa enzi za Mitume na manabii wa dahari na dahari! Kutaka na kupata haraka haraka ni fikra za ndoto ambapo mtu hulala na kuota kwamba amepata kila kitu, pesa, gari, jumba, mali na akawa tajiri kama mfalme! Lakini akiamka kutoka usingizini katika ndoto zake, hujikuta hali ni ile ile alivyokuwa awali!Tafadhali tuwe wavumilivu.

Kila mtu ana siku yake na wakati wake wa kupata riziki aliyopangiwa na Mwenyezi Mungu! Tabia hizi za kutaka kuchuma na kuvuna haraka haraka zimeleta majanga na masaibu mengi maishani. Angalia siku hizi visa vimekithiri vya ujambazi, ugaidi, ujangili, uporaji, wizi, utekaji nyara, kudai malipo haramu, dhuluma, ufisadi na kila utukutu wa kusaka mali mpaka unashindwa umwamini nani na usimwamini nani!! Kila mtu msakamali! Anayesaka mali pia akishapata mali husakwa na kusakamwa na mali yake aliyosaka kwa kuwadhulumu wengine!Ndugu wapenzi, tuwe watu waadilifu, watulivu wenye akili zilizomakinika.

Tuige hulka na silika za kobe mnyama aendaye polepole hadi mwisho wa safari yake! Kobe huishi miaka mingi duniani kwa sababu hana papara! Hizi papara na pupa hazileti ufanisi katika maisha!!! Wallah Bin Wallah ni Mwandishi Mlezi wa Kiswahili na Mkurugenzi wa WASTA KITUO CHA KISWAHILI kilichoko Ngong Matasia Nairobi Kenya

  • Tags

You can share this post!

Kundi la Malenga Wamilisi na Kiswahili ni chanda na pete

Messi aisaidia Argentina kufuzu kwa robo fainali kipute cha...