• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Pasta Ezekiel ni mweupe kama pamba, Kamati ya Seneti sasa yaamua

Pasta Ezekiel ni mweupe kama pamba, Kamati ya Seneti sasa yaamua

NA WINNIE ATIENO

KAMATI ya Seneti inayochunguza vifo vilivyotokea Shakahola, Kaunti ya Kilifi, imemwondolea lawama mhubiri Ezekiel Odero kuhusu madai ya kuficha maiti katika kituo chake cha New Life Prayer Center kilicho eneo la Mavueni.

Wakiwa katika harakati za kuthibitisha taarifa zinazomhusisha mhubiri huyo na mauaji ya Shakahola ambapo zaidi ya watu 400 walipoteza maisha, kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Tana River, Bw Danson Mungatana, ilisema haikupata chumba cha kuhifadhia maiti wala makaburi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Akizungumza katika kanisa hilo ambako kamati hiyo ilipiga kambi kuhakiki taarifa za mashahidi, alisema sehemu zilizoshukiwa kuhifadhi au kuzikwa maiti zimebainika kuwa na matumizi tofauti kabisa.

“Tumegundua hakuna chumba cha kuhifadhia maiti, badala yake ni chumba cha mitambo ya kompyuta (server room). Pale palipodaiwa kuwa ni makaburi tuligundua ni eneo la ujenzi. Kuna mambo tulitaka kuyafumbua na tumemhoji zaidi ili aeleze mambo ambayo hayaeleweki. Tunaondoka mahali hapa tukiwa tumeridhika kuwa hakuna kilichofichwa. Kila kitu kiko wazi na tumekagua kila sehemu tuliyotaka,” akasema Bw Mungatana.

Baada ya serikali kuanza kumchunguza mhubiri Paul Mackenzie ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya watu wengi huko Shakahola, uvumi ulienea katika maeneo ya umma kwamba Bw Odero alikuwa akiwazika waumini wake waliokufa katika kanisa lake na wengine kusafirishwa hadi Shakahola.

Uvumi huo ulitokana na hali kwamba, waumini wengi wagonjwa hutembelea kituo hicho kwa ajili ya maombi na ilidaiwa kuwa baadhi yao hawatoki huko wakiwa hai.

Uchunguzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai dhidi ya mhubiri huyo ulihusu madai kwamba kanisa hilo linahusika na ulanguzi wa fedha haramu na mauaji ya halaiki ambapo miili ilidaiwa kusafirishwa hadi msitu wa Shakahola.

Bw Mungatana alisema kuwa, maelezo mapya kuhusiana na mauaji ya Shakahola, yanatarajiwa kufichuliwa wakati kamati hiyo itatoa ripoti yake wiki hii.

“Tunahitimisha uchunguzi wetu wiki hii na tutatangaza ripoti yetu Alhamisi. Masuala yote yatawekwa wazi kwenye ripoti hiyo kwa Wakenya,” alisema.

Kamati hiyo ilifanya ziara yake Mavueni kwa mwaliko wa Bw Odero ambaye aliwataka waende kubaini taarifa ambazo zimetolewa dhidi yake, alipohojiwa Ijumaa iliyopita.

Siku hiyo hiyo, kamati ilihoji DCI faraghani kutokana na uzito wa ripoti za uchunguzi zinazoendelea.

Bw Mungatana alisema DCI pia imewaalika kuwatembelea kutafuta ukweli na wananuia kuwa katika makao yao makuu leo.
Bw Odero ambaye aliandamana na mhubiri Pius Muiru jana, alisema anashukuru kwamba alipewa nafasi ya kuwaambia Wakenya ukweli.

“Hatimaye ukweli umewekwa wazi. Ninafurahi kwamba Seneti iliitikia mwaliko wangu kuthibitisha madai,” akasema.

Maseneta walitembelea pia studio yake ya runinga na redio ambazo yeye hutumia kupeperusha mahubiri yake na ukumbi wa kanisa ambalo husitiri watu 45,000 kwa wakati mmoja.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Waraibu wa asali wanavyouziwa mchanganyiko wa sukari na...

Mwanamume ashtakiwa kwa kumteka nyara mkewe

T L